Jaji Kiongozi aiomba TAKUKURU kuwachunguza Mahakimu, Majaji waliotuhumiwa na DC Chuachua

NA DIRAMAKINI

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa zilizotolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Dkt. Rashid Chuachuadhidi ya Mahakimu na Majaji.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 22, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Artemony T.Vincent.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Januari 22, 2023 wakati wa sherehe za uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe.Dkt.Rashid Chuachua amenukuliwa na vyombo vya habari kuwa kuna baadhi ya Majaji na Mahakimu wanajihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili kwa kupokea rushwa kwa njia ya miamala ya simu.

"Kufuatia tuhuma hii, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, amemuagiza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mhe.Rose Ebrahim kuwasilisha hoja hii kwa Uongozi wa TAKUKURU wa Mkoa huo kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya tuhuma hiyo ili kubaini ukweli.

"Ikithibitika pasipo na shaka kwamba tuhuma hizi zina ushahidi wa kutosha, na bila ya kuathiri hatua nyingine zitakazochukuliwa na vyombo husika, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa watumishi hao watakaothibitika kutenda kosa hilo.

"Ni matumaini ya uongozi wa Mahakama kuwa waliotoa tuhuma watakuwa tayari kuthibitisha ili sheria ichukue mkondo wake bila kumuonea mtu yeyote au kuchafua taswira ya Mhimili wa Mahakama na watumishi wake,"ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Post a Comment

0 Comments