MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR:Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinajivunia kuwa sehemu ya maendeleo Zanzibar

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

MAPINDUZI ya Zanzibar husherehekewa kila mwaka ifikapo tarehe 12 Januari. Sherehe za mapinduzi huambatana na matukio mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kimaendeleo kama uzinduzi na ufunguzi wa shule mpya, hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi ya maji, barabara nakadalika.

Vilevile, sherehe za Mapinduzi hupambwa na sanaa na michezo ikiwemo kombe la Mapinduzi katika mpira wa miguu.

Mwaka huu Simba na Yanga zimetolewa mapema na fainali itapigwa baina ya Singida Big Stars ya Singida na Mlandege ya Zanzibar. Hivyo, sherehe za Mapinduzi hufana kwelikweli na huwavutia watu wengi wa ndani na nje ya Zanzibar.

Kiini cha Mada

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Tanzania ni taasisi ya Umma ya Elimu ya juu ambayo inajivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya Zanzibar ambapo madhumuni ya Mapinduzi ni kuhakikisha Zanzibar inajiletea maendeleo katika sekta zote na Elimu ikiwemo.

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilianzishwa mwaka 1992 kwa Sheria ya Bunge namba 17 kwa lengo la kutoa elimu ya juu kwa njia Huria, Masafa na mtandao.

Tangu kipindi hicho ambacho ni miaka 30 sasa Wanzanzibari wanapata elimu ya juu kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Katika kusherehekea miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinajivunia kuwa sehemu ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar kwa kutoa mchango wake wa kukuza na kuimarisha rasilimali watu, utafiti, ushauri wa kitaalamu, ugunduzi na ubunifu. Tunaweza kuthibitisha haya kama ifuatavyo:

Mosi: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kina matawi Unguja na Pemba ambayo yanatoa huduma kwa Wazanzibari katika ngazi zote za elimu ya juu.

Ni dhamira ya Mapinduzi kuona Wanzanzibari wanapata elimu ya juu kwa gharama nafuu wakiwa popote pale mijini na mashamba.

Pili: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupitia walimu na wanafunzi wanafanya utafiti katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii na uchumi wa buluu.

Kupitia tafiti hizo, kunapatikana masuluhisho ya changamoto zinazokabili sekta hizo na pia kuibua fursa za ajira kwa vijana na jamii nzima ya Wanzanzibari.

Zipo Tasinifu na Tazmini nyingi kutoka kwa wahitimu zilizowasikisha masuala mbalimbali ya Zanzibar. Tasnifu na Tazmini hizo zinapatikana mtandaoni kupitia OUT Repository.

Pia, wapo wahitimu waliotafiti katika sekta binafsi, mazingira, ujasiriamali, usafirishaji, lugha ya Kiswahili, elimu, afya, miundombinu nakadhalika. Tafiti hizo zinatumiwa na watunga sera katika kuandaa sera nzuri zinazoiletea Zanzibar maendeleo ya kasi.

Tatu: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimekuwa kikitoa wahitimu wa fani mbalimbali ambao ni sehemu ya watumishi wa Umma.

Watumishi hao wapo katika sekta mbalimbali wakitumikia katika nafasi tofauti tofauti. Wapo viongozi waandamizi, wapo viongozi maafisa,watumishi wa kawaida katika sekta ya umma na binafsi wakitoa huduma kwa wananchi.

Huduma hizo katika elimu, afya, maji, utalii, biashara, hoteli na ukarimu. Alumni wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni miongoni mwa watumishi wanaofanya kazi nzuri kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Mifano ipo mingi kuitaja sintowahi kuimaliza. Maendeleo endelevu ndiyo azma kuu ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nne: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa mchango wake katika kuitangaza Zanzibar kimataifa. Katika matangazo yetu tunaeleza bayana kwamba tuna matawi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Unguja na Pemba.

Hii husaidia sana katika kuimarisha utalii, huduma za hoteli na ukarimu kutokana na wingi wa watalii na wageni wanaotembelea Zanzibar.

Wahitimu wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Miradi (Master of Project Management) wakitunukiwa Shahada yao na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania,.Mhe.Mizengo Peter Pinda.(hayupo pichani) Novemba 25, 2021 wakati wa mahafali ya 40 ya chuo hicho yaliofanyika katika Uwanja wa Mao Zedung Wilaya ya Mjini Unguja jijini Zanzibar.

Mwaka 2021 Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilifanya mahafali yake Zanzibar. Kupitia mahafali hiyo tuliweza kuitangaza Zanzibar katika nchi nyingi duniani. Huu ni mchango wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kuiletea Zanzibar Maendeleo.

Tano: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa mchango wake kuunga mkono azma ya Mapinduzi katika eneo la hamasa.

Kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Masoko ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania tumekuwa tukiandaa mashairi, tenzi, insha na makala kuhamasisha jamii katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Kazi hii hufanyika kupitia mitandao ya kijamii, redio, magazeti na televisheni. Kazi hii ni endelevu na inaendelea kila siku na hata insha hii ni sehemu ya hamasa kwa Wazanzibari kujiletea maendeleo

Hitimisho

Kimsingi, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinajivunia kuwa sehemu ya kuchagiza maendeleo ya Zanzibar kupitia maeneo mbalimbali yaliyowasilishwa kwa muhtasari katika insha hii.

Sisi wana Huria tutaendelea kutoa mchango kwa kuzalisha wataalamu wenye viwango vya juu vya ubora ili kuendelea kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Tutaendelea kubuni program ambazo ni muafaka kwa Zanzibar na hasa uchumi wa buluu. Hii itasaidia na kuendeleza kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi pamoja na viongozi wote wanaomsaidia. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape afya njema waendelee kuleta maendeleo kwa kasi zaidi.

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Post a Comment

0 Comments