Waziri.Prof.Mkenda:Tunafanya kazi kwa kushirikiana kuelekea mageuzi ya Sera ya Elimu na Mitaala

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara ya Elimu Bara na ile ya Zanzibar zinafanya kazi kwa kushirikiana katika suala la mageuzi ya Sera ya Elimu na maboresho ya mitaala ili kuwawezesha vijana wa pande zote mbili kupata ujuzi na stadi zitakazowasaidia kujiari ama kuajiriwa na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza Januari 11, 2023 jijini Zanzibar katika hafla ya ugawaji wa vishkwambi kwa walimu wa Zanzibar vilivyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema, Prof.Mkenda anaamini mapendekezo yatakayotolewa na Serikali baada ya kupokea maoni ya wadau yatashabihiana isipokuwa tu pale ambapo mazingira yatahitaji kuwe na tofauti.
"Kuhusu suala la mageuzi ya elimu naamini hakutakuwa na tofauti kubwa kati ya Elimu ya Bara na ya Visiwani kwa kuwa kazi ya mapitio ya Sera na mitaala imefanywa kwa ushirikiano wa pande zote mbili," amesema Prof. Mkenda.
Kuhusu ugawaji wa Vishikwambi, Prof. Mkenda amesema Serikali imetoa vishkwambi 6,600 kwa walimu upande wa zanzibar ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kugawa vishkwambi kwa walimu wote nchini katika kutambua umuhimu wa TEHAMA kwenye ufundishaji na ujifunzaji.

Waziri huyo amesema kitendo cha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kutoa motisha ya kompyuta kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitachochea juhudi za wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na hivyo kuwa tayari kujenga Taifa.
Prof.Mkenda ameongeza kuwa, baadhi ya wanafunzi waliopata kompyuta wa kidato cha sita ambao walifaulu vizuri masomo ya sayansi ni wanufaika wa "Samia Scholarship" hivyo watasomeshwa bure na Serikali kupitia mpango huo.

Katika hafla hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amegawa vishkwambi kwa walimu na kompyuta mpakato kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita kutoka skuli za Zanzibar ili kuwapa motisha wanafunzi kuendelea kufanya vizuri.Dkt. Hussein Mwinyi amesema Serikali yake itaendelea kuipa kipaumbele cha kwanza Sekta ya Elimu kwa kuwa maendeleo yoyote hayawezi kupatikana bila ya Elimu.

Mwinyi ameongeza kuwa anaamini vishkwambi hivyo vitasaidia kupiga hatua kwenye suala zima la TEHAMA katika sekta ya Elimu.
"Ili nchi iwe na wataalamu ni lazima iwekeze kwa kiasi kikubwa kwenye elimu hivyo tutajipanga kutoa mafunzo kwa walimu waliopo na kuongeza wengine ili tuzalishe wataalamu watakaoiinua nchi," amesema Rais Mwinyi.
Kwa upande wake Mhe. Lela Mohamed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ameshukuru kwa kupokea vishkwambi hivyo 6,600 na kwamba vitagawiwa kwa Walimu wa shule za Msingi na Sekondari za umma ili wavitumie kama zana za kufundishia na kujifunzia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news