Mawaziri watano 'wanasa' Morogoro

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro mkoani Morogoro,Gerold Mlenge amewatuhumu mawaziri watano, kwa kuwa sehemu ya uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na wao kumiliki mifugo mingi wilayani humo.

“Sasa isifike mahali nikaita press nikawataja kwa majina, muende mkanong'onezane watoe, huku Morogoro Vijijini hatuna asili ya mifugo, sisi kazi yetu ni kulima, hatutaki migogoro, hatutaki migogoro ya wakulima na wafugaji;

Mlenge ameyasema hayo kwenye ziara ya Waziri wa Maji, Jumaa Uweso wakati akizindua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika Kata na Kijiji cha Lundi wilayani humo.

Kiongozi huyo wa chama alimuomba,Waziri Aweso kuchukua majina ya mawaziri hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mheshimiwa Albert Msando ambaye tayari ameshafikishiwa taarifa na majina hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.

Amesema,kiasili wilaya hiyo haina eneo la ufugaji ila ni kilimo, lakini kwa sasa kuna wafugaji wengi kuliko wakulima ambao ni wavamizi na wamekuwa wakiwasumbuwa wakulima ikiwemo kuharibu vyanzo vya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza katika Kijiji cha Lundi amesema, changamoto ya maji hasa kuharibika kwa vyanzo vyake zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara zinazoshabihiana na suala la mifugo ambapo aliahidi kuliwasilisha lalamiko lao la mawaziri watano wanaomiliki mifugo wilayani humo kama lilivyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

“Nimepewa ombi maalum na viongozi hapa, juu ya changamoto ya mifugo, nikiri kulipokea na nitalipeleka kama lilivyo kama mlivyotaka, mimi ni muathirika pia, moja ya changamoto kubwa sana ni kuharibika kwa vyanzo vya maji, hivyo nitaliwasilisha kwa sababu hata kule kwenye uzinduzi wa Bwawa la Nyerere, Mheshmiwa Rais alieleza uelekeo na nitalifikisha ili kuhakikisha jambo hilo linapata ufumbuzi,"amesema Waziri Aweso.

Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilayani humo, Mhandisi Grace Lyimo akisoma taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Maji Lundi amesema, mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi milioni 492.8 ambao ukikamilika kwa asilimia 100 utatimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutoa huduma bora za maji kwa wananchi 4,604 wa vijiji vya Ng’ongola na Lundi kwenye vitongoji saba.

Pia amesema, mradi huo umeanza kutekelezwa tangu Januari 17,2022 na ulitarajiwa kukamilika Julai 16, 2022 ambapo umeongezewa muda na kutakiwa kukamilia Februari 7,2023 kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.

Amesema, chanzo cha maji cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 264,000 kwa siku na mahitaji ya maji katika vijiji hivyo viwili ni lita 230,200 kwa siku.

Mhandisi Lyimo amefafanua kuwa, kazi kuu zilizopangwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la lita 150,000, ujenzi wa nyumba mbili za mitambo ya kusukuma maji, kunganisha umeme wa TANESCO, kazi ya kuchimba, kulaza bomba na kufikia urefu wa kilomita 19, ununuzi wa bomba za laini kuu na bomba za kusambaza maji, kujenga vituo 17 vya kuchotea maji vijijini na ukarabati wa vituo sita vya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news