Rais Dkt.Mwinyi: Benki Kuu ni mdau muhimu Sekta ya Maendeleo Zanzibar

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni mdau muhimu wa sekta ya maendeleo Zanzibar na ni mshauri mzuri kwa masuala ya uchumi wa nchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Emmanuel Tutuba na Gavana mstaafu wa BoT, Prof. Florens Luoga na uongozi wa BoT, wakiwa katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo Januari 18,2023, alipofika na uongozi wake kwa mazungumzo na kujitambulisha.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Januari 18, 2023 Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na Gavana mpya wa benki hiyo, Emmanuel Mpawe Tutuba, aliyefika kujitambulisha tangu alipoteuliwa Januari 7, 2023 na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua na ushirikiano mzuri na BoT wakati wote pamoja na kupata ushauri mzuri wa uendeshaji wa uchumi wa Zanzibar.

Pia ameongeza Zanzibar imepata mafanikio makubwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania na kueleza ushirikiano wa taasisi mbili hizo umejenga ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao ipasavyo.
Rais Dkt.Mwinyi amemuahidi Gavana huyo kushirikiana naye kwenye majukumu yake kwa kipindi chote cha uongozi wake na kumshauri kuendeleza alipofikia mtangulizi wake.

“Nikupe ahadi tu ya ushirikiano wetu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tukiwa wadau muhimu wa kazi zinazofanywa na Benki Kuu, tupo tayari kushirikiana vya kutosha kwa masuala yote yanayohitaji ushirikiano wetu,” ameahidi Rais Dkt.Mwinyi.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemuahidi Gavana huyo kufanyanaye kazi bega kwa bega kwa msaada mkubwa wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi zake, na kuongeza kwamba kazi nzuri ambayo ilifanywa na mtangulizi wake, Prof.Florens Luoga ilileta mafanikio makubwa kwa Serikali.
Akizungumzia changamoto za uchumi wa Dunia,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemweleza Gavana Tutuba kwamba washirikiane kutafuta ufumbuzi mzuri wa kuzigeuza changamoto hizo kuwa fursa ili zilete tija kwa taifa pamoja na kuziangalia kwa kuzidhibiti ili zisiathiri uchumi wa nchi.

Rais Dkt.Mwinyi amemuahidi Gavana huyo kushirikiana naye kwenye majukumu yake kwa kipindi chote cha uongozi wake na kumshauri kuendeleza alipofikia mtangulizi wake.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemshuru Gavana aliyemaliza muda wake, Prof. Florens Luoga kwa ushirikiano wake alioutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi chote cha utumishi wake kwa Taifa, na kueleza kwamba wakati mwingine hakuishia tu kwenye ngazi ya wizara bali alifika hadi ngazi za juu katika kufanikisha majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu.
Naye Gavana Tutuba amesema, Benki Kuu ya Tanzania ni chombo cha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kinachofanya kazi zake kwa pande zote mbili za Muungano katika kusimamia masuala ya kiuchumi na sera za fedha kwa Zanzibar na Bara.

Amesema,Serikali zote mbili zipo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi kwa kudhibiti mfumko wa bei duniani uliochangiwa na athari kubwa za kupanda kwa bei za mafuta ambayo inaathiri zaidi sekta ya usafirishaji kwa wananchi.

Gavana Tutuba ametumia fursa hiyo kuzipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wake kuwapunguzia makali yanayotokana na athari hizo.
Naye Gavana wa zamani, Prof. Florens Luoga ametumia fursa hiyo kumuaga Rais Dkt.Mwinyi baada ya kumaliza muda wa utumishi wake kwa Benki Kuu ya Tanzania pia ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano iliyoutoa kwake muda wote wa utumishi wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news