Rais Dkt.Mwinyi:BMF endeleeni kuboresha mifumo ya afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi

NA DIRAMAKINI

MSARIFU wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation (BMF), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameueleza uongozi wa taasisi hiyo kuendelea kuboresha mifumo ya afya kwenye taasisi yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Msarifu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Menejimenti na watumishi wa taasisi hiyo, mkutano huo umeyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo Januari 18,2023.(Picha na Ikulu).

Aidha, ameutaka uongozi huo kuangalia kwa upana jinsi ya kukamilisha miundombinu ya vifaa tiba pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano itakayotoa huduma bora kwa walengwa na kuboresha utendaji kwa kuongeza nguvu kazi za ajira ili kutanua wigo kwenye taasisi hiyo.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na uongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation Ikulu jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Msarifu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi,akimkabidhi Tuzo,Cheti na Fedha Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Dkt.Ellen Mkondya-Senkoro, wakati wa mkutano wake na Manejimenti na Watumishi wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, uliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na taasisi hiyo katika kuimarisha huduma bora za afya pamoja na kupongeza juhudi za BMF katika utendaji kazi wake nchi nzima, Bara na Zanzibar.

Mbali na kusifu jitihada zinazochukuliwa na uongozi kwa kuisimamia vyema taasisi hiyo, pia Dkt. Mwinyi amewataka watendaji na wafanyakazi wa BMF kuanzisha bima ya afya kwa lengo la kwenda sambamba na mahitaji ya wananchi.
“Wenzetu kule Bara wameshaanza kutoa bima ya Afya na sisi Zanzibar tunakaribia kuanza,” Rais Dkt.Mwinyi aliuelezea uongozi wa BMF.

Katika hatua nyingine Rais Dkt Mwinyi aliwatunuku vyeti, tuzo na fedha taslimu wafanyakazi waliofanya vizuri kwenye taasisi hiyo kwa kipindi cha utumishi wao pamoja na kuwapongeza.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya BMF, Balozi Tuvako Manongi amesema, bodi yao imeendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali zikiwemo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wadau wa maendeleo wakiwemo wafadhili kutoka sekta za umma na binafsi pamoja na wachangiaji binafsi katika kuhakikisha wanapata rasilimali fedha.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa BMF, Dkt.Ellen Senkoro amesema taasisi imekusudia kuvitekeleza vipaumbele vyake vinne ikiwemo kuufanyia tathmini ya Mpango Mkakati uliopo wa taasisi hiyo ili kuongeza ubunifu na wigo wa kuanzisha miradi mipya baada ya mikongwe iliopo kukamilika kwa asilimia 50.

Aidha, alieleza wanaboresha utendaji wa taasisi hiyo kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kupunguza gharama za uendeshaji na kufanyakazi kwa weledi na kuongeza kuwa walifanikiwa kutekeleza miradi mikubwa na midogo kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 ambayo iliboresha huduma za afya kwa mikoa 25 ya Bara na mitano ya Zanzibar, ikiwemo kuongeza rasilimali watu, kuimarisha miundombinu ya majengo na vifaa tiba pamoja na kukabiliana dhidi ya mapambano ya Ukimwi, kifua kikuu na UVIKO 19.

Hata, hivyo ameahidhi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya taasisi hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kufanikisha dira ya taasisi yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Msarifu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Balozi Tuvako Manongi, baada ya kumalizika kwa mkutano na Menejimenti na Watumishi wa taasisi hiyo uliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.

Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation iliasisiswa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news