RAIS WETU DKT.SAMIA, KWELI HANA ROHO MBAYA

NA LWAGA MWAMBANDE

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, Mheshimiwa Tundu Lissu ambaye amekuwa akiishi uhamishoni baada ya jaribio la kutaka kumuua, alipopigwa risasi na watu wasiojulikana mwaka 2017 jijini Dodoma, amerejea nyumbani Januari 25, 2023.

Lissu baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam alipokelewa na wafuasi wa chama hicho kabla ya kuelekea viwanja vya Mwembe Yanga vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini humo kuzungumza nao.

Tukio hili la kihistoria, ni moja wapo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuendelea kudumisha umoja, mshikamano, upendo na maridhiano katika jamii ya Watanzania tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2021.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,Rais Dkt.Samia ni miongoni mwa viongozi wachache wa karne hii ambao wana hofu ya Mungu,wanathamini utu na kuheshimu maoni ya wengine kwa mustakabali na ustawi bora wa Taifa letu. Endelea;

1.Kweli hana roho mbaya,
Kwa aliyoyafanya haya,
Asemaye mambo haya,
Ndiye huyu Tundu Lissu.

2.Kakaa sana Ulaya,
Sababu ya roho mbaya,
Na watu wengi wabaya,
Ndiye huyu Tundu Lissu.

3.Ila Rais Samia,
Vema amemfanyia,
Hiana imeishia,
Karudi nyumbani Lissu.

4.Yake tunakumbukia,
Vibaya limfanyia,
Angeweza kuishia,
Alinusurika Lissu.

5.Ikabidi kukimbia,
Ugenini kuishia,
Vile walimtishia,
Huyu ndugu yetu Lissu.

6.Rais wetu Samia,
Huko alimfikia,
Kwenda kumsalimia,
Ubelgiji kwa Lissu.

7.Akamhakikishia,
Ni salama Tanzania,
Aweze kukaribia,
Huyu ndugu yetu Lissu.

8.Tayari ameingia,
Hapa kwetu Tanzania,
Wengi wameshangilia,
Kurudi kwa ndugu Lissu.

9.Hivyo anamsifia,
Rais wetu Samia,
Vile amemfanyia,
Huyu ndugu yetu Lissu.

10.Hili lipate ingia,
Ni mwema sana Samia,
Mema anatufanyia,
Na sisi yanatuhusu.

11.Wengine Watanzania,
Nchi waloikimbia,
Vema wakaturudia,
Kama livyorudi Lissu.

12.Kwao hapa Tanzania,
Amani tumetulia,
Kusiwepo kukimbia,
Mbona amerudi Lissu.

13.Heri tunawatakia,
Wasikize ya Samia,
Ambayo atufanyia,
Amethibitisha Lissu.

14.Heri Rais Samia,
Yako tunafurahia,
Watufaa Tanzania,
Yako mengi yatuhusu.

15.Ipige kazi Samia,
Twende mbele Tanzania,
Pazuri tutafikia,
Ufanyayo yatuhusu.

16.Lissu kwako Tanzania,
Siasa tajifanyia,
Heri tunakutakia,
Ya Samia yakuhusu.

17.Wengi tunafurahia,
Mwenzetu Mtanzania,
Kwako unakurudia,
Karibu nyumbani Lissu.

18.Amani twakutakia,
Ukiwepo Tanzania,
Uweze kufurahia,
Karibu nyumbani Lissu.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news