Serikali yatoa maagizo kwa viongozi wa elimu

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Festo Dugange amewataka viongozi wa elimu ngazi ya shule, kata,halmashauri na mikoa kutokaa ofisini bali wafuatilie ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kushauriana na walimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa katika masomo yote.

Dkt.Dugange ametoa maelekezo hayo Januari 9,2023 mkoani Njombe katika mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu msingi na sekondari uliowakutanisha viongozi wa elimu ngazi zote.

“Viongozi wa elimu jielekezeni zaidi kufuatilia ufundishaji wa walimu darasani na kutatua kero za walimu kwenye maeneo yao ya kazi na mhakikishe mnaimarisha uwajibikaji wa watumishi wote katika ngazi zote ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi,”amesisitiza Dkt.Dugange.

Amewataka walimu kujiwekea malengo yao binafsi katika masomo wanayofundisha na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa katika somo lake analofundisha.

Dkt.Dugange amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa na anaendela kuwekeza katika elimu ambapo ameendelea kutoa kiasi cha shilingi bilioni 29.82 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila ada.

Aidha, Dkt.Dugange ameeleza kuwa, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya nchi nzima kwa ajili ya kupokea wanafunzi kidato cha kwanza mwaka 2023 ambao wameanza kupokelewa shuleni.

Hadhalika, amesema Serikali inaendelea kuwekeza pesa nyingi katika sekta ya elimu kupitia miradi mbalimbali kama mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wa shilingi trilioni 1.2, mradi wa kuimarisha Elimu ya Msingi BOOST wa shilingi trilioni 1.15.

Wakati huo huo, Dkt.Dugange ameeleza mafanikio ya katika Sekta ya Elimu ambapo idadi ya wanafunzi wa elimumsingi wameongezeka kutoka wanafunzi 11,877,565 mwaka 2016 hadi 15,609,931 mwaka 2022 pia idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita iliongezeka kwa asilimia 35.86 kutoka 131,362 mwaka 2016 hadi 178,473 mwaka 2022.

Pia, ameeleza ongezeko la ufaulu wa mitiani ambapo Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi umeongezeka kutoka asilimia 70.40 mwaka 2016 hadi asilimia 79.62 mwaka 2022.

Ufaulu wa Mtihani wa Kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 70.35 mwaka 2016 hadi asilimia 87.30 mwaka 2021 na Kidato cha Sita, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 97.94 mwaka 2016 hadi asilimia 99.87 mwaka 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news