TAARIFA KWA UMMA KUHUSU NDEGE ZINAZOTUA NA KURUKA KWENYE MAENEO YA HIFADHI

NA MWANDISHI WETU

HIVI karibuni kumekua na taarifa za uzushi na upotoshaji zinaendelea kutolewa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wenye nia ovu ili kuzua taharuki kuwa ndege zinazoruka na kutua katika maeneo ya hifadhi zinasafirisha wanyamapori na rasilimali nyingine zinazolindwa na kuhifadhiwa kisheria.

Taarifa hizo sio za kweli tunaomba wananchi mziipuze. Kama tunavyofahamu Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii zikiwemo Hifadhi za Taifa 22, Mapori ya Akiba 22, Mapori Tengefu 29, Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi za Misitu, maeneo ya kihistoria na urithi wa dunia, Hifadhi za Bahari na fukwe, maziwa makuu, mito na maeneo mengine mengi ya asili.

Maeneo haya ya vivutio yamekuwa yakitembelewa na watalii wa aina mbalimbali na kuliingizia Taifa fedha za kigeni pamoja na kuzalisha fursa za ajira.

Aidha, watalii wengi wamekua wakiitembelea Tanzania kutokana na juhudi kubwa za kutangaza utalii zilizofanyika ambazo zimekua kichocheo cha shughuli mbalimbali zikiwemo za utalii wa picha, safari za parachuti (balloon), kutembea nyikani, kupanda milima, utalii wa fukwe na utalii wa utamaduni.

Kutokana na umuhimu wa shughuli hizo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imefanya maboresho makubwa ya kufungua na kukarabati miundombinu ya Utalii vikiwemo viwanja vya ndege, barabara na miundombinu mingine muhimu katika maeneo ya hifadhi ili kuwezesha uendelevu wa shughuli za uhifadhi pamoja na kuiwezesha Sekta Binafsi kutoa huduma ya usafiri wa ndege zinatua na kuruka kwa nyakati tofauti zikiwa zimebeba watalii kutoka katika viwanja vikubwa hususani Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Abeid Amani Karume International Airport , Zanzibar.

Kwa muktadha huu, Wizara ya Maliasili na Utalii inawahakikishia Watanzania kuwa viwanja vyote vya ndege vilivyoko katika maeneo ya hifadhi viko salama na vinatumika kwa shughuli za usafirishaji wa watalii wanaotoka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Aidha, Wizara iko makini kuhakikisha matumizi sahihi ya viwanja hivyo kwa wageni wote wanaoingia na kutoka katika maeneo ya hifadhi.

Tunawaomba wananchi muwe watulivu na kuwa makini na watu wanaotoa taarifa za upotoshaji na za kichochezi zisizo rasmi kuhusu ndege na matumizi ya viwanja hivyo.

Aidha, tunawaomba wananchi mnapoona matumizi yasio sahihi msisite kutoa taarifa kwenye vituo vyetu vya uhifadhi, vituo vya Polisi au ofisi za Serikali zilizo katika maeneo yenu ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali zetu.

Tumerithishwa, Tuwarithishe!

Imetolewa na; -
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
Januari 10,2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news