Waziri Kairuki atoa siku 14 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)

NA ANGELA MSIMBIRA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki ametoa siku 14 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuwasilisha wizarani orodha ya taarifa sahihi na za kina za walimu wote nchini.

Taarifa zinazotakiwa kuwasilisha ni zile zinazoeleza kwa kina kila mwalimu amejiriwa lini, na nafasi aliyoajiriwa nayo, nafasi au cheo alicho nacho kwa sasa, lini amepandishwa cheo na kama hakupandishwa kwa nini na kama mwalimu alijiendeleza na alijiendeleza katika ngazi ipi na eneo lipi.

Kairuki ametoa agizo hilo Januari 19, 2023, jijini Mwanza wakati wa kufungua kikao kazi cha mapitio ya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usambazaji wa elimu nchini.

Amesema, TSC inapaswa kuandaa TANGE za Utumishi wa Walimu na kuziwasilisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI ndani ya wiki mbili kuanzia sasa lengo likiwa ni kutatua changamoto za walimu.

"Tume hakikisheni mnaandaa TANGE itakayobainisha, mwalimu aliajiriwa lini, nafasi aliyopo, cheo alichonacho kwa sasa, alipanda lini cheo, kwa nini hakupanda cheo, lini alijiendeleza ili Ofisi ya Rais-TAMISEMI ishirikiane na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora kutatua changamoto za walimu nchini,"amesema.

Amesema, kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kujua taarifa sahihi za mwalimu, taarifa za kielimu,uzoefu kazini, taarifa za ajira yake, cheo alichonacho sasa na mwaka aliopandishwa cheo lengo likiwa ni kubaini changamoto za upandaji wa madaraja kwa walimu nchi nzima.

Aidha, Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaonya wakurugenzi na maafisa utumishi wanaopoka haki za mtumishi wakiwepo walimu bila sababu.

"Badala ya kutumia lugha ya kudhalilisha, kuwanyanyasa na kuwafanyia vitendo visivyofaa, basi mnachopaswa kufanya ni kuwaelimisha watumishi ili wajue kanuni za utumishi wa umma na nyaraka mbalimbali za utumishi,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news