Mchungaji Dkt.Eliona Kimaro apewa msamaha ulioacha maswali magumu KKKT

NA DIRAMAKINI

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani limetangaza msamaha kwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Dkt.Eliona Kimaro.

Msamaha huo ambao haujaeleza wazi haina ya kosa ambalo alilifanya umekuja leo Februari 19, 2023 ikiwa zimesalia siku kadhaa kabla ya Mchungaji Dkt.Kimaro kumaliza likizo ambayo alidai kupewa awali.

“Semina yetu ilikuwa ya wiki mbili, lakini leo niliitwa Ofisi ya Msaidizi wa Askofu na nilikuwa na kikao na Msaidizi wa Askofu na Mkuu wa Jimbo la Kaskazini, nimepewa barua ya likizo ya siku 60 na kuambiwa nirudi Machi 17 na nikirudi nikaripoti Makao Makuu ya Dayosisi,”alikaririwa Mchungaji Kiongozi wa kanisa,Dkt.Eliona Kimaro awali.

Dkt.Kimaro siku ya Januari 16,2023 alitangaza kuwa, Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) ilimpa likizo ya miezi miwili bila kuweka wazi sababu za likizo hiyo.

Licha ya kupewa likizo ya miezi miwili, Dkt.Kimaro alitakiwa kuripoti makao makuu baada ya likizo yake itakapomalizika, jambo ambalo liliibua taharuki kwa waumini wa kanisa hilo na hata baadhi ya waumini wa KKKT Kijitonyama wakaandamana wakiomba uongozi wa kanisa hilo umrudishe Dkt.Kimaro.

Msamaha huo umetangazwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Gehaz Malasusa leo kupitia ibada ya Jumapili katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

“Sote ni Wakristo, lakini wengine tumeitwa ili tuwaongoze katika kazi ya Mungu na hawa ni wachungaji, tuwatunze, tuwasaidie, tuwaombee na tuwapende.

“Mchungaji Kimaro, ndugu yangu kama ulivyoomba na mimi nasema kwa niaba ya washarika umesamehewa, endelea kutafakari, endelea kukaa karibu na Mungu shetani kamwe asituondoe katika mstari, naomba nikushike mkono, Baba Askofu nimekubariki, pole sanasana sanasanasana maana najua pia umeumia sana endeleeni kukaa chini ya miguu ya Mungu.

“Tumeiona huduma yenu na Mungu awatie nguvu, nitaendelea kuwaombea kwa sababu ni jukumu langu na nyinyi bado ni watoto wangu, Mungu awabariki sana,”amefafanua Askofu Malasusa.

Akizungumza wakati wa ibada hiyo Mchungaji Dkt.Kimaro ameomba radhi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt.Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote uliojitokeza wakati huu ambao amekuwa likizo.

“Naomba radhi kwa mkuu wa kanisa Askofu, Dkt.Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote ambao ulijitokeza katika mitandao na kwenye vyombo vya habari kwa wakati huu ambao nimekuwa likizo ya faragha,”amesema Dkt.Kimaro.

Pia, amemshukuru Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt.Alex Malasusa kwa upendo na kazi kubwa ya kumtunza kichungaji.

Msamaha huu unakuja ikiwa tangu awali, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt.Fredrick Shoo aliwataka washarika wa KKKT Usharika wa Kijitonyama uliopo Dayosisi ya Mashariki na Pwani jijini Dar es Salaam kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho kunaonekana hali ya mvutano.

Dkt.Shoo alitoa wito huo Januari 17, 2023 ikiwa ni saa chache baada ya baadhi ya washirika wa kanisa hilo kuandamana kanisani hapo na kuuomba uongozi wa KKKT umrudishe Mchungaji Kiongozi wa kanisa,Dkt. Eliona Kimaro ambaye alitangaza kuwa amepewa likizo ya miezi miwili.

"Niombe utulivu kwa washarika na kwa Wakristo ambao wamesikia habari hizo za uamuzi amabao umefikiwa na Dayosisi yake. Tambua kuwa Dayosisi ina vyombo vyake vya maamuzi, na bila shaka jambo lenyewe linaendelea kufanyiwa kazi na dayosisi husika.

"Na sisi ambao sasa tunapokea taarifa kama hizi, tunaendelea kufuatilia na kupata taarifa zaidi kuhusu jambo hili ambalo linaonesha kuleta usumbufu na maitikio au reactions mbalimbali tofauti tofauti kutoka kwa watu mbalimbali,"amefafanua Dkt.Shoo.

Dkt.Kimaro amekuwa maarufu zaidi kupitia huduma za ibada ambazo amekuwa akiendesha ikiwemo Morning and Evening Glory: “The School of Healing: Shule ya Uponyaji”.

Ibada hizo huwa zinafanyika kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa kwa maana ya Morning Glory: Saa 11:30-12:30 Asubuhi, Evening Glory: Saa 12:00-2:00 Jioni.

Kwa mujibu wa ushirika huo, Shule ya Uponyaji ni mafundisho yenye msingi wa Kibiblia yenye lengo la kuwezesha watu wa rika na madhehebu yote kuponywa Kiroho, Kimwili, Kiakili na Kifikra kwa njia ya kumjua Mungu na kufahamu kusudi la Mungu kwa mwanadamu na kuishi maisha yanyoendana na kusudi la Mungu na viwango amavyo Mungu amevikusudia kwake.

Msingi wa Shule ya Uponyaji ni kutoka Methali 1: 1-7; ambao uanlenga kujua matendo makuu ya Bwana ili kujua hekima na adabu, kutambua maneno ya ufahamu, kufundishwa matendo ya busara katika haki, hukumu na adili, kuwapa wajinga werevu. Kuwapa vijana maarifa na hadhari, kuwaongezea elimu wenye hekima, na wenye ufahamu mashauri yenye hekima.

Shule hiyo ya Uponyaji inatambua umuhimu wa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla na kuwa vijana wengi wanahitaji kupewa maarifa na hadhari ili kuwajenga katika msingi ambayo itawasaidia kujituma katika kufanya maendeleo ambayo yataleta mabadiliko makubwa kwa Tanzania na Ulimwengu.

Mafundisho haya huwa yanalenga kuwasaidia vijana kupata maarifa ya kuona fusara zenye Baraka za Kimbingu na hadhari katika maisha yao.

Pia Shule ya Uponyaji huwa inaambatana na Ushauri wa Kichungaji unaofanyika kila mwezi Septemba lengo likiwa ni kutoa ushauri nasaha ili kuwafungua watu na kuponya jeraha zao, Majadiliano ili kutoa fursa ya kupokea shuhuda mbalimbali na kuona jinsi ambavyo watu wamefanikiwa ili kuwatia moyo wengine na kupata mbinu, ujuzi na maarifa ya kufanikiwa kupitia misingi ya Kibiblia.

Aidha, Shule ya Uponyaji huwa inawaleta watumishi wa kitheologia toka madhehebu mbalimbali, wachumi, wafanyabishara na wataalamu wa fani mbalimbali ili kuhudumia kanisa la Mungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news