Waziri Prof.Mkenda aagiza uchunguzi shule za Cornelius,Thaqaafa,Mnemonic na Twibhoki kwa udanganyifu

NA MWANDISHI WyEST

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mhe. Profesa Adolf Mkenda amemuagiza Kamishna wa Elimu kufanya uchunguzi wa kina kwa shule nne zilizobainika kufanya udanganyifu mkubwa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022.
Prof. Mkenda amesema hayo alipokutana na Wazazi na walezi wa Wanafunzi waliofutiwa matokeo ya Mtihani wa Kidato nne 2022 wa Shule ya Sekondari Thaqaafa ya Jijini Mwanza kwa ajili ya kuwasikiliza.

Amezitaja shule hizo kuwa ni Cornelius ya Kinondoni ya Dar es Salaam, Thaqaafa ya Mwanza, Mnemonic ya Zanzibar na Twibhoki iliyoko Mara na kumtaka Kamishna huyo kuchukua hatua kali kulingana na ripoti ya uchunguzi huo.
Mkenda amesisitiza wazazi kuwalea watoto katika maadili ili watambue kuwa udanganyifu si mzuri na una madhara makubwa katika upande wa haki, maadili na uweledi.

"Tunapowapeleka watoto shule tunataka wajifunze waelewe ili baadae waje watumikie taifa. Sasa mtu anakuja kuwa daktari au mhandisi au rubani kwa kuiba mtihani, madhara yake ni makubwa sana," ameongeza Mkenda.
Mkenda amewapa pole wazazi na kuwataarifu kuwa mitihani hiyo imefutwa na hivyo kilichopo ni kurudia mitihani.

"Kuhusu kurudia mtihani tumewasikiliza maombi yenu, ninashukuru kuwa hamna anayesema ameonewa sote tunakubaliana kuwa kulikuwa na udanganyifu na hivyo niseme matokeo yamefutwa na kikubwa ni maombi ya kurudia mtihani. Hili tunalichukua tutawasiliana nanyi baada ya kulifanyia kazi kwani ni suala la kibajeti pia," amefafanua Mkenda.
Naye Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akiwa katika kikao hicho amesema Serikali haitalea shule zinazofanya udanganyifu wa mitihani na kuongeza kuwa wanafunzi wanatakiwa wapimwe kwa uwezo na sio kwa kudanganya.
Katika maelezo yao yaliyotolewa kupitia Mwenyekiti wa wazazi hao, Patrick Msagati wameomba Serikali kuwahurumia na kuruhusu matokeo kuachiliwa au kuwapa nafasi ya kurudia mtihani.

"Tunaomba Serikali ichukue hatua kali kwa shule kama hizi kwani zimetusababishia madhara makubwa sisi kama wazazi na watoto pia. Ikiwezekana shule hizi zifungiwe," amesema Michael Zayumba, mmoja wa wazazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news