OUT KUFANYA MAPITIO YA MITAALA

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania-Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Deus Ngaruko amesema Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinafanya kazi kubwa ya kupitia upya mitaala (Curriculum Review) yake yote ya shahada, shahada za uzamili na uzamivu ili ziweze kujibu mahitaji ya jamii ya sasa na baadae.
Sambamba na mapitio ya mitaala pia chuo kinafanya kazi ya kuhuisha ithibati yake (Re-accreditation) ambayo ni takwa la sheria chini ya TCU ambalo hutekelezwa kila baada ya miaka mitano kwa vyuo vikuu vyote.
Prof. Ngaruko, ambaye ndiye mratibu mkuu wa mradi wa HEET wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Wativa, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara za kitaaluma na waratibu wa programu za masomo kuhusiana na ufuatiliaji kifani wa wahitimu (Tracer Study) wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania walipo na wanachokifanya.

Mafunzo hayo yamefanyika Februari 2, 2023 makao makuu ya OUT Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Mitaala itakayopitiwa upya inafika idadi ya sabini na tano (75) ambapo kupitia msaada wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tumepata fedha kupitia mradi wa Mabadiliko ya Kiuchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET) kwa ajili ya mapitio ya mitaala hiyo.

"Tumeshakutana katika mikutano kadhaa inyohusiana na kupitia mitaala, pia tumepata mafunzo mengi kutoka kwa wataalamu wa mradi wa HEET kutoka wizarani. Mafunzo haya ya leo ni mwendelezo wa kuhakikisha hakuna mtu anaachwa nyuma katika kufanikisha upitiaji wa mitaala yote ya chuo chetu.

"Kila mtu anashirikishwa katika kazi hii adhimu kwa chuo na taifa kwa jumla. Tunapomaliza hapa washiriki wote wanakwenda kutoa mafunzo na maelekezo kwa wafanyakazi wa Idara na vitengo vyao ili kuhakikisha tunapata tija na ufanisi wa hali ya juu katika utekelezaji wa mradi wa HEET,”amesema Prof. Ngaruko.
Prof. Ngaruko amesema kuwa, chuo kitapata manufaa makubwa ikiwemo kupitia mitaala yake iweze kuendana na hali ya ajira na kujiajiri kwa sasa ambapo pia zinaweza kuanzishwa kozi mpya ili kukidhi mahitaji hayo.

Aidha, ameeleza kwamba ufuatiliaji kifani wa wahitimu utaleta mabadiliko katika mitaala kwa kiwango cha asilimia 25 na jamii itarajie program zilizoboreshwa na kuimarishwa katika kutoa wahitimu wenye ujuzi na maarifa kulingana na mahitaji ya jamii.

Vilevile upitiaji huu wa mitaala utasaidia sana katika kufanikisha kazi ya kuhuisha ithibati ya chuo.
Kwa upande wake mratibu wa kitengo cha Huduma za Ujifunzaji na Ufundishaji cha OUT, Dkt. Yohana Lawi, amesema kuwa ufuatiliaji kifani wa wahitimu utasaidia kupata taarifa za wahitimu wetu waliomaliza miaka ya nyuma walipo kwa sasa katika ajira za kujiajiri au kuajiriwa. Lengo kuu ni kutaka kufahamu utendaji wao kupitia ujuzi na maarifa walioyapata kupitia elimu ya OUT.

“Taarifa za wahitimu ni muhimu kwa taasisi, itasaidia kupitia upya mitaala na kumuwezesha muhitimu ajaye kuwa na elimu bora itayomuwezesha kumudu mazingira na mahitaji ya jamii ya sasa na baadae.

"Pia itatusaidia kuangalia elimu yetu ni kwa kiwango gani inamwezesha mhitimu kujiajiri yeye mwenyewe na kutengeneza fursa ya ajira kwa watu wengine, hili ndiyo lengo kuu la mradi wa HEET. Lakini tunatarajia kupata taarifa kutoka kwa waajiri ambao ndio wanufaika wa wahitimu wetu ili kufahamu wahitimu hao kama wanakidhi mahitaji ya waajiri,"amesema Dkt.Lawi.
Naye Mkuu wa Idara Jografia, Utalii na Ukarimu ya OUT, Dkt. Halima Kilungu, ambaye ni miongoni mwa wasimamizi na wawezeshaji wa kazi ya mapitio ya mitaala amesema kwamba wanakwenda kufuatilia wahitimu wa OUT wapo wapi, wanafanya nini ili taasisi iweze kuwa na kanzi data itakayowezesha kujua kama walichosoma wahitimu wake kinawasaidia kwenye kuleta maendeleo yao na taifa kwa jumla.

Aliendelea kusema kuwa mojawapo ya hitaji la mradi wa HEET ni chuo kuboresha mitaala yake ili kizalishe wahitimu ambao wanahitajika kwenye soko la ajira, wahitimu wenye uelewa wa kutosha na wawe wanaajirika na zaidi kujiajiri.

Ufuatiliaji kifani utakiwezesha Chuo kujua soko la ajira na mazingira ya kujiajiri yanahitaji wahitimu wenye ujuzi na maarifa gani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news