Rais Dkt.Mwinyi:Taasisi za dini zina mchango mkubwa nchini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema taasisi za dini zina mchango mkubwa kwa Serikali hasa kwenye jukumu zima la kuendeleza amani Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Hindi Sunni Jamaat Zanzibar, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Nizar Mohammed (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kumpongeza Februari 2, 2023. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, taasisi hizo ndizo zinazowalea vijana kiimani, weledi, ujasiri na uzalendo kwa taifa na viongozi wao jambo ambalo linaimarisha amani na uthubutu wa kufikia maendeleo.

Ameyasema hayo Februari 2, 2023 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na uongozi wa Jumuiya ya Sunni Jamaat waliofika kujitambulisha.

Amesema, taasisi binafsi na za kidini zina jukumu la kuisaidia Serikali kuendeleza huduma za jamii pia ameishukuru jumuiya hiyo kwa juhudi za kuendeleza elimu Zanzibar.

Pia amezitaka jumuiya za dini kuendelea kuishauri Serikali kwa mawazo yatakayojenga na kuleta ufanisi kwenye misingi ya maendeleo ya taifa, hata hivyo aliishukuru taasisi hiyo kwa mchango wanaoutoa kwenye sekta ya elimu.

Rais Dkt.Mwinyi amezungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya elimu zikiwemo uhaba wa vifaa vya maabara, maktaba, kuongeza madawati, kompyuta na vitabu, pia kuondoa mikondo kwa wanafunzi. Hata hivyo, amesema Serikali ya Awamu ya Nane imejenga skuli 48 kati ya hizo 10 ni za ghorofa.

“Kwa hatua tuliyofikia matokeo yanaweza yasionekane leo, maana ukianza kuigeuza elimu faida yake itaonekana miaka mingi baadae,”amefafanua Rais Dkt.Mwinyi.

Amesema, Serikali pia inafanya utafiti wa kina kutafuta suluhu ya wanafunzi wengi kufeli na kuweka mikakati imara itakayoinua Sekta ya Elimu Zanzibar.

“Safari hii tumeamua kufanya utafiti maana changamoto za elimu ni nyingi mno kila kona, huwezi kuziepuka, kuanzia idadi ya wanafunzi kwenye madarasa ndio maana tunajenga skuli mpya ili kupunguza idadi ya wanafunzi wengi madarasani,”amesema.

Amesema, Serikali pia inaangalia upya mfumo wa elimu ambao wanafunzi wengi huanza msingi, lakini wanaoingia vyuoni ni wachanche hivyo inaangalia kundi la katikati linalofeli ambalo ni kubwa.

Wana jumuiya hao wamemshukuru Rais Dkt.Mwinyi kwa juhudi ya kuipambania sekta ya elimu nchini na kueleza kuwa wameshuhudia mafanikio makubwa ndani ya miaka miwili ya uongozi wake hasa kwenye kutoa kipaumbele kuimarisha huduma za jamii.

Walitumia fursa hiyo kumsifu kwa uongozi wake mahiri ambao waliueleza kwamba unaendelea kudumisha amani iliyopo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news