Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo, mahakama ya 'mafisadi' mbioni

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imezitaka taasisi za umma kubadili mifumo ya zamani ya utendaji na utoaji huduma kwa wananchi kwa kuanzisha mifumo ya kisasa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji wao kuenda na kasi ya matumizi ya teknolojia.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizindua Bendera ya Mahakama Zanzibar, wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, iliyofanyika Februari 13,2023, katika viwanja vya Mahakama Kuu Zanzibar Tunguu Wilaya ya Kati Unguja na kushoto kwa Rais ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah na kulia kwa Rais ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Khamis Juma. (Picha na Ikulu).

Maagizo hayo yametolewa Februari 13, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria, Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema, wakati huu wa sayansi na teknolojia mifumo ya uendeshaji taasisi kwa kutumia karatasi na kalamu imepitwa na wakati, hivyo alizitaka taasisi za umma zikiwemo taasisi za sheria na wadau wake kubadili mifumo ya utendaji wao ili kuendana na kasi ya teknolojia.
Amesema, matumizi ya TEHAMA hurahisisha utendaji na kuondosha usumbufu pia kusaidia jitihada za Serikali za kukuza uchumi wa nchi na kuimarisha ustawi wa jamii kwa kuokoa fedha nyingi zinazogharamia shughuli zinazotekelezwa kwa mifumo ya zamani na badala yake gharama ya fedha hizo zitaelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumzia haki mtandao mahakamani, Rais Dkt.Mwinyi amesema ni muhimu kwa ujenzi wa taasisi bora za kisheria, kwani mfumo unaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani.
Hata hivyo, ameipongeza Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mara ya kwanza kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kusajili mawakili ambao alieleza kwa sasa watafungua mashauri na kufuatilia uendeshaji wa mashauri hayo wakiwa nyumbani, vijijini au ofisini.

Amesema, mfumo huo wa kisasa utasaidia kuokoa muda unaotumika kwenye taasisi za sheria kufanyia kazi nyingine za kuinua vipato vyao, kuimarisha uwazi, uwajibikaji, utawala bora, ukusanyaji mzuri wa mapato na kuimarisha uchumi wa nchi pamoja na kusaidia kukuza imani ya wananchi na wawekezaji wa ndani na nje kwenye vyombo vya sheria.
Akizungumiza faida za matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za sheria, Dkt.Mwinyi amesema, ni usikilizaji wa haraka wa mashauri na kutolewa maamuzi, upatikanaji wa takwimu sahihi, ufuatiliaji bora na usimamizi bora wa mashauri.

“Kwa kupitia haki mtandao, hakutakuwa na ulazima kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu kusafirishwa kwenda Pemba kusikiliza mashauri, kwani mashauri hayo yatasikilizwa na kuamuliwa kwa mfumo wa TEHAMA tu, shahidi hatalazimika kufika kwenye jengo la mahakama kutoa ushahidi.
"Inaweza kuandaliwa mifumo ya kutoa ushahidi wake kupitia hata simu yake tu ya mkononi, utaratibu huu mienendo ya kesi itapatikana kwa haraka,”amefafanua Dkt.Mwinyi.

Rais,Dkt.Mwinyi ameahidi kutoa kipaumbele kwa bajeti ya matumizi ya TEHAMA kwa Mahakama Kuu Zanzibar ili kuimarisha miundombinu ya taasisi za sheria nchini, na kusema kwamba Serikali itatumia zaidi ya bilioni nne kwa ujenzi wa majengo manne ya Mahakama Kuu na za wilaya kwa Unguja na Pemba ambazo zinaendana na mifumo ya TEHAMA.

Aidha, ameitaka mahakama hiyo kupitia taasisi zake kujipanga na kuwasilisha serikalini mpango kazi na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa azima hiyo.
Pia ametoa wito kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kupitia Ofisi ya Wakala wa Serikali Mtandao kuzisimamia na kuzishauri ipasavyo taasisi zote za sheria katika kufikia lengo hilo la haki mtandao nchini.

Hata hivyo, aliitaka Mahakama kushirikiana na wadau wengine wa haki kwa maboresho yoyote kwenye mhimili wa Mahakama alisema yataleta matokeo chanya yenye ufanisi kwa ushirikiano imara na wadau.
Akizungumzia uanzishwaji wa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Rais Dkt.Mwinyi alisifu jitihada zilizofikiwa na Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa hatua waliyofikia na kueleza kufarijika kwake kusikia tayari wameunda kamati ya wataalamu kwa ajili ya kusimamia na kuratibu mchakato wa kuanzishwa mahakama hiyo.

Alieleza kuanzishwa kwa mahakama hiyo, kutaisaidia Serikali mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi na rasilimali za umma ambayo huzorotesha uchumi wa nchi na ustawi wa jamii hali aliyoieleza inarejesha nyuma juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alisema karne ya 21 inazitaka taasisi zote na watendaji wake kuwa na mabadiko ya fikra na kimtazamo yanayoendana na teknolojia iliyopo duniani, na kuongeza kuwa mabadiliko ya teknolojia kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar yatasaidia utoaji wa haki na kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuleta mageuzi makubwa ya mabadiliko ya utendaji wao. 

Hivyo, aliwataka majaji kutumia jitihada za ziada ili kuendana na kasi ya huduma mtandao kwa sasa.
Naye Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, alisema maadhimisho ya siku ya sheria ni kuanza mwaka mpya wa mahakama na kueleza miongoni kwa mikakati ya mabadiliko yao kwenye ufanisi wa utendaji kazi wao ni kuwafikia wananchi kwa haraka, kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwa karibu nao kwa ajili ya kuwahudumia pamoja na kutoa mahakama rafiki zenye huduma za haraka.
Maadhimisho ya sheria yaliambatana na wiki ya sheria iliyoanza Febuari 6, mwaka huu kwa kutekelezwa shughuli mbalimbali za kisheria ikiwemo kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya sheria, kutambua mchango wa makaadhi kwa kutunukiwa vyeti vinara bora watoaji haki.

Pia kupokea mawakili wapia, kuzindua mfumo wa kuwasajili mawakili kwa njia ya mtandao pamoja na kuhitimishwa kwa matembezi yaliyoandaliwa na taasisi ya “Zanzibar Maisha bora Foundation” yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Mama Mariam Mwinyi yakiwa na kauli mbiu “Kupinga vita dhidi ya Udhalilishaji wa Kijinsia.”
Aidha, maadhimisho ya Sheria pia yalihudhuriwa na ujumbe kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania ulioongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Juma yalikuwa na kauli mbiu, “Haki mtandao ya kukuza uchumi na Ustawi wa jamii” ni maadhimisho ya 12 tokea kuanzishwa kwake mwaka 2012.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news