REA:Mikataba ambayo tumeingia imegawanyika katika makundi makuu matatu

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema, mikataba ambayo wameingia hivi karibuni imedhamiria kupelekea nishati ya umeme vijijini ingawa imegawanyika katika makundi makuu matatu.

Mhandisi Saidy ameyasema hayo leo Februari 17, 2023 na UFM Radio ya jijini Dar es Salaam ambapo amebainisha kuwa,nishati hiyo itawafikia wananchi wengi nchini.

"Mikataba ambayo tumeingia yote inapeleka nishati vijijini, lakini tumeigawa katika makundi makuu matatu.Kundi la kwanza ni kupeleka umeme kwenye vitongoji 1,522 ambavyo vitapata umeme kwa maana ya wananchi wa vijijini na mradi huo wa kwanza utaunganisha wateja karibu 88,800.

"Zoezi la pili ni kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo na maeneo ya kilimo, huu ni mradi umelenga kwa wajasiriamali wa kati vijijini ambao utapelekwa kwenye maeneo 336, lakini utaunganisha wateja 18,968.

"Huu ni mradi unaokwenda kwenye machimbo na kwenye maeneo ya makazi ambayo wachimbaji wanaishi, hili ni eneo kubwa la pili.

"Na eneo la tatu ni mradi wa kupeleka kwenye vituo vya afya na pampu za maji, huu utapeleka kwenye vituo 396 kwa ujumla wake na hii miradi miwili ya kupeleka kwenye vituo vya afya na kwenye machimbo utakwenda nchi nzima, lakini wa umeme kwenye vitongoji utagusa mikoa tisa tu,"amefafanua Mhandisi Saidy.

Februari 14, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan
wakati akishuhudia utiaji saini mikataba ya kuimarisha gridi ya taifa na kusambaza umeme vijijini alisema, miradi hiyo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.9 ni muhimu kwa wananchi kwa kuwa itaimarisha huduma za maji, kilimo, afya na hivyo kuleta maendeleo.

Shirika la Umeme (TANESCO) liliweka saini mikataba sita kwa ajili ya miradi 26 ya gridi imara na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iiliweka saini mikataba 14 kwa ajili ya miradi ya kupeleka umeme kwenye migodi midogomidogo na maeneo ya kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news