TANZANIA YA KWANZA KUSAINI MKATABA WA KITUO CHA HUDUMA YA DHARURA CHA MAAFA MIONGONI MWA NCHI ZA SADC

NA MWANDISHI WETU 

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu na oparesheni za dharura za kanda.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu ) Mhe. George Simbachawene (aliyekaa) akisaini Mkataba wa Kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda (SHOC) Februari 23, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma (kulia) ni Katibu Mkuu Ofisi hiyo Dkt. John Jingu.(Picha na OWM).

Akizungumza leo Februari 23,2023 wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dodoma,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.
Aliongeza kuwa, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi tarehe 21 Juni, 2021.

“Lengo la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa,"amefafanua.
Aliendelea kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi; Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.
Mwakilishi wa Sekretarieti ya Nchi za SADC ambaye pia ni Mwanasheria, Dkt. Phiness Matto akifafanua jambo baada ya utiaji saini Mkataba wa Kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda (SHOC) Februari 23, 2023 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.

Awali mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt.Phiness Matto, alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri itavyowezekana.

“Natoa Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea nchi 11 kusaini mkataba huu,"amefafanua Dkt.Matto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news