Afariki akiwa anafanyiwa maombi

NA DIRAMAKINI

“Mtoto alikuwa anasumbuliwa na vidonda visivyouma mdomoni, anapiga mswaki, lakini haviumi, damu inatoka masikioni, lakini ukimuuliza anasema hayaumi, damu inatoka puani ukimuuliza anasema haviumi kwa kweli huo ugonjwa ulituchanganya hata sisi;

Hayo yamesemwa na baba mzazi wa Consolata Pius mwenye umri wa miaka 16, Bw.Charles Pius ambapo, binti huyo anadaiwa kufariki wakati akiwa nyumbani kwa mchungaji akifanyiwa maombi katika Kijiji cha Mkuyuni Kata ya Magamba Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Pius amedai mtoto wake alikuwa akisumbuliwa na maradhi ambayo hata baada ya kumpeleka hospitali hayakuweza kutambulika, ndipo mchungaji alipoomba kumchukua kwa ajili ya kumfanyia maombi.

Baba huyo alisema,siku ya kwanza toka mchungaji huyo wa kanisa mjini hapa amchukue alilala nyumbani kwake na siku ya pili ndipo umauti ulipomkuta.

Mchungaji Peter James anayedaiwa kumchukua mtoto huyo, amedai alimchukua kwa lengo la kumsaidia kutokana na mazingira magumu aliyokuwa akiishi kijijini hapo.

James amedai alipigiwa simu na familia ya mtoto huyo kwenda nyumbani kumfanyia maombi, baada ya kukuta anaishi kwenye mazingira magumu wao kama kanisa walimchukua kwa ajili ya kumuhudumia ikiwa ni pamoja na kumfanyia maombi.

Kwa upande wao baadhi ya majirani wanadai walichanganyikiwa kuona mtoto huyo anatapika damu, ndipo walipochukua uamuzi wa kumpigia mchungaji kwa lengo la kwenda nyumbani kumuombea.

“Mimi nilipiga simu kwa wachungaji, hao ambao tunasali nao wakaja wakamuombea, bibi yake akasema mchukueni muende naye hukohuko, tutakua tunakuja tunamuona wakamchukua, wakakaa naye kule ndani ya siku mbili hali ikabadilika hadi alipokutwa na umauti.

“Huyu binti ni jirani yangu na alikuwa Dar es salaam anafanya kazi, alipokuja hakukaa siku nyingi kama siku tatu hivi akaja kwangu akasema, babu mimi madonda yamenitoka mdomoni, wala hayaumi hayawashi naomba unioneshe dawa ya madonda nikamwambia sielewi msaada ni kwenda zahanati ukapate ushauri,"alidai.

Baadhi ya majirani walieleza kuwa, awali hali ilivyokuwa mbaya ilibidi aende zahanati na kwenye vipimo wakasema anaumwa malaria na U.T.I.

Walidai, binti huyo baadaye alipewa dawa na rufaa kwenda hospitali kubwa alipofika akapewa kitanda ikaonekana damu hana ikabidi watu wakajitolee damu na kweli walikwenda baada ya hapo aliruhusiwa akarudi.

“Alikaa siku ya kwanza ya pili ugonjwa tena ukarudi, ndio mchungaji akaja hapa wakamuombea na kumbeba kumpeleka kwake alishinda juzi, jana akafariki,”alidai mmoja wa majirani hao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkuyuni Kata ya Magamba Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Getani Chambanenge amekiri kutokea kwa tukio hilo, huku akiwataka wananchi kutolihusisha na imani za kishirikina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news