Mahakama yawaachia huru vigogo Chama cha Walimu Tanzania (CWT)

NA DIRAMAKINI

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru waliokuwa viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambao ni Katibu, Deus Seif na Mtunza Hazina ,Abubakary Alawi baada ya kushinda rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi yao.

Wawili hao wameachiwa huru mbele ya Jaji Kisanya baada ya kushinda rufaa hiyo iliyotokana na uamuzi uliotolewa Juni 28,2022 katika Mahakama ya Kisutu ambapo walipatikana na hatia ya makosa ya matumizi mabaya ya ofisi na uchepushaji fedha.

Katika uamuzi wa Jaji Kisanya amebainisha kuwa, amejiridhisha bila kuacha shaka kwamba, ushahidi uliotolewa mahakamani Kisutu haukuwatia hatiani moja kwa moja wawili hao, hivyo anawaachia huru.

Juni 28,2022 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu nchini Tanzania (CWT), Deus Seif na Mweka Hazina wa chama hicho, Abubakari Allawi walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela.

Ni baada ya kupatikana na hatia ya kutumia madaraka yao vibaya kwa kuchepusha shilingi milioni 13.9 mali ya chama hicho.

Hukumu hiyo ilisomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi yao ya uhujumu uchumu namba 39/2021 ilipoitwa.

Akitoa Hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate alisema, mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao na kila mmoja atatumikia kifungo cha miezi sita jela.

"Mbali na adhabu hii, mshtakiwa kwa kwanza (Seif) utakapomaliza kutumikia kifungo chako utatakiwa kuilipa fidia CWT ya shilingi milioni 7,590,000, kwa upande wa mshtakiwa wa pili (Allawi) wewe utakapomaliza kutumikia kifungo hicho utatakiwa kuilipa fidia CWT kiasi cha shilingi milioni 6.2, haki ya kukata rufaa ipo wazi," alisema Hakimu Kabate.

Awali, jopo la mawakili watatu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) wakiongozwa na Iman Nitume, waliomba Mahakama hiyo itoa adhabu kali dhidi ya washtakiwa hao kwa mujibu wa sheria walivyoshtakiwa nayo.

"Kulingana na makosa waliyotenda na uhalisia wa nafasi za uongozi walizokuwa nazo CWT, ambapo waliaminiwa na walimu ambao walikuwa wanatoa michango yao kwa ajili ya chama hicho lakini wao walitumia hela za chama kwa maslahi yao binafsi,"alidai Wakili Nitume.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili wa utetezi Nesto Mkoba aliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu wateja wake kwa sababu ni wagonjwa, wanategemewa na familia zao na pia wanawahudumia wazazi wao wenye umri zaidi ya miaka 80.

Aidha, katika kesi ya msingi, Seif na Allawi, walidaiwa kati ya Oktoba 3, 2018 na Novemba 6, 2018, katika ofisi za CWT zilizopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa chama hicho, walitumia mamlaka yao vibaya kwa kujipatia shilingi milioni 13, 930,693.

Shtaka la pili, siku na maeneo hayo, Seif na Allawi, walidaiwa kwa kutumia madaraka yao vibaya na kwa manufaa yao wenyewe walichepusha fedha kiasi cha shilingi milioni 13.9 ambazo ni mali ya CWT.

Wakati huo huo, viongozi hao walidaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya kulipia tiketi za ndege pamoja na kulipia gharama za malazi kwa ajili ya safari ya kwenda Cape Verde kuangalia mpira wa miguu.

Pia inadaiwa kuwa mwaka 2018, huko Cape Verde kulikuwa na mechi ya mpira wa miguu kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), waliokuwa wanacheza na Timu ya Taifa ya Cape Verde.

Hata hivyo, washtakiwa kwa kufanya hivyo, walidaiwa kwenda kinyume na vifungu vya 29 pamoja na 31 vya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news