WALA USIIGEIGE-2:Binti Unayo thamani yako daima

NA LWAGA MWAMBANDE

UKITAFAKARI kwa kina neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu kuanzia Kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo, utabaini kuwa, kusudi la Mungu kwako Binti awaye yeyote ni chanzo bora cha wewe kuwa na ndoto, dira na maono katika maisha yako.

Maombi na kulisoma, kulitafakari na kulifanyia kazi neno la Mungu ni silaha ulinzi tosha kwa binti mwenye thamani. (Picha na loveworldusa).

Ndiyo maana mara nyingi watumishi wa Mungu wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kujitambua na kuifahamu thamani yako, kwani pasipo kuijua thamani yako huwezi kujitunza, kujilinda na hata kujiheshimu.

Kama ilivyo kwa kitu ambacho hujui thamani yake ni vigumu sana kukitunza, vivyo hivyo hata ubinti wako pia usipotambua thamani ya maisha yako huwezi kuyatunza, kuyajali, kuyalinda na hata hutoweza kujiheshimu.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, binti anayeitambua na kuifanyia kazi thamani yake si tu kwamba anajijengea heshima kuu, bali ni baraka kubwa kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Chini, Mwandande anakushirikisha utenzi ambao ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam. Endelea;


1. Ongeza thamani yako,
Huo upekee wako,
Fanya yako peke yako,
Wala usiigeige.

2. Huo upekee wako,
Jua ndio lulu yako,
Katika eneo lako,
Wala usiigeige.

3. Fasheni zote si zako,
Zingine ni za wenzako,
Chagua za peke yako,
Wala usiigeige.

4. Ulipo uwepo wako,
Usiwe kama wenzako,
Kwani uko peke yako,
Wala usiigeige.

5. Yaangaze macho yako,
Katika eneo lako,
Upi upekee wako?
Wala usiigeige.

6. Ijenge thamani yako,
Ukifanya mambo yako,
Tofauti na wenzako,
Wala usiigeige.

7. Wakikita cha kwako,
Hicho wakipate kwako,
Tofauti na wenzako,
Wala usiigeige.

8. Kule usikokuwako,
Kwa ile thamani yako,
Kujae masikitiko,
Wala usiigeige.

9. Kama mtaani kwako,
Uko wewe na wenzako,
Jitokeze peke yako,
Wala usiigeige.

10. Upekee wema wako,
Na hiyo heshima yako,
Kutokelezea kwako,
Wala usiigeige.

11. Unawaona wenzako,
Heshima yao si yako,
Mavazi yao si yako,
Wala usiigeige.

12. Tafuta eneo lako,
Onyesha ubora wako,
Na tena wa peke yako,
Wala usiigeige.

13. Una upekee wako?
Tofauti na wenzako?
Au sawa na wenzako?
Wala usiigeige.

14. Huko kwenye kazi yako,
Ukifanya mambo yako,
Tofauti na wenzako?
Wala usiigeige?

15. Pengine chuoni kwako,
Na wanachuo wenzako,
Una upekee wako?
Wala usiigeige.

16. Unawaona wenzako,
Mara huku mara huko,
Fwata msimamo wako,
Wala usiigeige.

17. Huo msimamo wako,
Hata upekee wako,
Ni utambulisho wako,
Wala usiigeige.

18. Ijenge brandi yako,
Wajue jamaa zako,
Wasilete yaso yako,
Wala usiigeige.

19. Huo uamuzi wako,
Kujenga brandi yako,
Uko mikononi mwako,
Wala usiigeige.

20. Leo hii ndiyo yako,
Kuanza hatua zako,
Kujenga thamani yako,
Wala usiigeige.

21. Unayo thamani yako,
Mbele yake Mungu wako,
Ni huo uhai wako,
Wala usiigeige.

22. Huo uumbaji wako,
Siyo sawa na wenzako
Una upekee wako,
Wala usiigeige.

23. Mwangalie Mungu wako,
Awe kiongozi wako,
Wala si hao wenzako,
Wala usiigeige.

24. Watu na waige kwako,
Huo upekee wako,
Wa hayo maisha yako,
Wala usiigeige.

25. Ujenge ubora wako,
Itunze thamani yako,
Tofauti na wenzako,
Wala usiigeige.

26. Wanaoiga wenzako,
Huonekana kituko,
Wewe usiende huko,
Wala usiigeige.

27. Fungua milango yako,
Baraka za Mungu wako,
Kwa hayo maisha yako,
Wala usiigeige.

28. Mungu wa kwako ni wako,
Ndiye Muumbaji wako,
Na utoshelevu wako,
Wala usiigeige.

29. Kwa hayo mapito yako,
Hata kujikwaa kwako,
Usiache utu wako,
Wala usiigeige.

30. Unayo mifano yako,
Hizo changamoto,
Mungu yu upande wako,
Wala usiigeige.

31. Kwani kwa mateso yako,
Yafanana na wenzako?
Yako ni ya kwako tu,
Wala usiigeige.

32. Mwangalie Mungu wako,
Mlilie Mungu wako,
Yeye ndiye jibu lako,
Wala usiigeige.

33. Unawaona wenzako,
Shida zao siyo zako,
Njia zao siyo zako,
Wala usiigeige.

34. Unaumwa tumbo lako,
Sababu maisha yako,
Usisikilize huko,
Wala usiigeige.

35. Wanavyoiga wenzako,
Watoke huko waliko,
Hayo yao siyo yako,
Wala usiigeige.

36. Na huo mwenendo wako,
Hata msimamo wako,
Waleta adui kwako,
Wala usiigeige.

37. Mungu Muumbaji wako,
Aona maisha yako,
Hata upekee wako,
Wala usiigeige.

38. Tabaki upande wako,
Awe kila kitu kwako,
Ufurahi kesho yako,
Wala usiigeige.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Utenzi huu ni sehemu ya Mafundisho ya Mchungaji Imani Oscar Katana (0752 352 116) wa Kanisa la Baptist la Moto Ulao lililoko Dege, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo ameyatoa katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya mabinti. Mashairi yatakujia katika sehemu saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news