MARBURG, TUNAWEZA KUISHINDA:Tuzingatie maelekezo na miongozo ya Serikali

NA LWAGA MWAMBANDE

MACHI 21, 2023 Waziri wa Afya,Mheshimiwa Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema, uchunguzi wa Maabara ya Taifa umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg, ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Marburg Virus Disease (MVD) katika Mkoa wa Kagera.

Picha na AfricaCDC.

Ugonjwa ambao umesababisha vifo vya watu watano na watatu wapo hospitalini, huku ugonjwa huo ambao hauna tiba mahususi, Waziri alisema hutibiwa kwa dalili anazokuwa nazo mgonjwa.

“Uchunguzi ambao tumeufanya katika Maabara yetu ya Taifa ya Afya ya Jamii umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa unaojulikana kama Marburg Virus Disease (MVD).

“Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu wa Marburg uligundulika kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1967 katika Mji wa Marburg na ndio asili ya jina la ugonjwa huu, ugonjwa huu ulishawahi kuripotiwa katika Nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya.

“Ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa majimaji ambayo yanaweza kuwa mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au mgonjwa mwenye dalili, maambukizi pia yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa,"alifafanua Mheshimiwa Waziri Ummy.

Hayo yalijiri baada ya, Machi 16, 2023 Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu huko jijini Dodoma kutangaza kuwa, watu watano wamefariki dunia na wengine wawili wakiwa hospitalini baada ya kuibuka kwa ugonjwa ambao bado haujajulikana huko Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Serikali ilitoa tahadhari kwa umma kuwa, ugonjwa huo umejitokeza katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega, Kata ya Maruku na Kanyangercko Vilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Prof. Nagu alisema, jumla ya watu saba wanasadikika walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ugonjwa huu wa Marburg tunaweza kuushinda, kubwa tuzidi kuzingatia maelekezo na miongozo ya wataalamu wa afya huku tukiendelea kumlilia Mungu atuondolee janga hilo. Endelea;

1.Imezuka huko homa, hatutaki liwe janga,
Kujikinga wamesema, sote twapaswa kulenga,
Vile tiba hii homa, ni sawasawa kudanga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

2.Ugonjwa kuuepuka, jua jinsi kujikinga,
Maiti mtu kushika, Marbug lomdunga,
Ee ndugu yangu epuka, bila ya vifaa kinga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

3.Na kugusanagusana, kwaweza kushusha kinga,
Na mikono kupeana, epuka unajikinga,
Busu kukumbatiana, hayo mambo ya kijinga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

4.Tunarudi kulekule, magonjwa mengi kukinga,
Kunawa mikono kule, na sabuni wajikinga,
Mara nyingi vilevile, usijekuleta janga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

5.Kula kugusa mizoga, wajisogezea janga,
Bora kula mbogamboga, mwili wazidi kukinga,
Kwa hili usijezuga, ukasingizia mwanga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

6.Dalili za homahoma, kuishiwa nguvu janga,
Kutokwa damu wasema, kote bila kujivunga,
Tapika harisha noma, sipitali wewe tinga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

7.Tiba hakika hakuna, muhimu ni kujikinga,
Nyemelezi ukiona, hospitalini songa,
Wataalamu kuona, huduma wataipanga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

8.Ndugu tumewapoteza, kwa kule ulikotinga,
Serikali metangaza, maeneo wayachunga,
Hata WHO wameweza, kutuma huko wakunga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

9.Vinginevyo hali shwari, mbele tuzidi kusonga,
Muhimu ni tahadhari, kwingine usijetinga,
Ikawa kwetu hatari, litangazwe liwe janga,
Hii homa Marburg, tunaweza kuishinda.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news