Rais Dkt.Samia amewapa heshima watumishi nchini-Waziri Kairuki

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imewapa heshima na thamani watumishi nchini.

Mheshimiwa Kairuki ameyasema hayo leo Machi 16, 2023 wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika Ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.

"Naomba kutumia nafasi hii ya kipekee kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jitihada anazozifanya katika kupunguza kero na malalamiko ya watumishi nchini,"amefafanua Waziri Kairuki.

Vile vile, Mheshimiwa Waziri Kairuki amesema, katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt.Samia, Taifa limeshuhudia watumishi wa umma wakipandishwa vyeo kwa mfululizo.

"Ambapo Mwenyekiti wa Baraza ameeleza kuwa kati yenu, watumishi wa tume 304 walipandishwa vyeo na watumishi 24 walibadilishiwa cheo au kazi baada ya kujiendeleza kielimu. Si hivyo tu hata walimu 160,888 mnaowahudumia walipandishwa vyeo kwa miaka miwili mfululizo (2020/21 na 2021/22).

"Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameweza kutoa vibali vya ajira katika kada mbalimbali ikiwemo kada ya ualimu. Sote tumeshuhudia katika kipindi cha utawala wake walimu 24,749 waliajiriwa ambapo mwaka 2020/2021 walikuwa walimu 14,949 na mwaka 2021/2022 walimu 9,800. Tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais; Mama Samia hoyeee,"amesisitiza Waziri Kairuki.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Kairuki ameipongeza Tume ya Utumishi wa Walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya kusimamia vema utumishi wa walimu wote nchini.

"Natambua kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu ndiyo iliyopewa dhamana ya kusimamia utumishi wa walimu ambao ni zaidi ya asilimia hamsini ya watumishi wa umma nchini. Hongereni sana kwa kazi nzuri,"amebainisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news