Serikali yaendeleza miradi mingi ya elimu

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendeleza miradi mbalimbali ya elimu nchini kwa ustawi bora wa sekta hiyo muhimu kwa jamii na Taifa.

Mheshimiwa Kairuki ameyasema hayo leo Machi 16, 2023 wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika Ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.

"Sote tumeshuhudia jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira thabiti ya kuendeleza elimu nchini kupitia kupitia miradi mbalimbali aliyoiasisi yeye mwenyewe.

"Kupitia Mradi wa Kuboresha elimu ya sekondari nchini (SEQUIP), Mheshimiwa Rais ameridhia kutumiwa kwa shilingi trilioni 1.2 kujenga shule mpya za sekondari 1,026 kuanzia mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2024/2025,"amefafanua Waziri Kairuki.

Mheshimiwa Waziri Kairuki amesema, hadi sasa jumla ya shule 242 zinaendelea kukamilishwa kujengwa. Aidha, kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha, jumla ya shule za sekondari 184 zitajengwa, shule moja katika kila halmashauri.

Amebainisha kuwa, kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na msingi (BOOST), Mheshimiwa Rais ameridhia pia kutumika kwa shilingi Trilioni 1.15 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/2023.

Waziri amesema,kupitia fedha hizo katika mradi wa BOOST, Serikali imepanga kujenga madarasa 12,000 na shule 6,000 kutekeleza Mpango wa Shule Salama.

Sambamba na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali kufikia asilimia 85 kutoka asilimia 76.9 ya sasa, walimu wa elimu ya awali kujengewa uwezo wa ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia ujuzi unaowiana na mtaala.

Pia utekelezaji wa Mpango Endelevu wa Mafunzo Kazini (MEWAKA) kwa walimu wa shule za msingi, kuwa na walimu wanaofikia viwango vinavyokubalika vya umahiri katika ufundishaji utakaopimwa na Wathibiti Ubora wa Shule,matumizi ya TEHAMA katika kufundishia pamoja na kuwa na halmashauri zinazokidhi vigezo vya utawala bora katika usimamizi wa masuala ya elimu.

"Nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kutoa kipaumbele kuendeleza sekta ya elimu na walimu. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais,"amesema Waziri Kairuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news