NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amesema Kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga kitakuwa kijiji cha mfano kwa vijiji vingine nchini kwenda kujifunza kutokana na kuwekewa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kusimamiwa vizuri.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akipokewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando alipowasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja Machi 22,2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
Dkt.Mabula amesema hayo Machi 22,2023 wakati wa zoezi la kukabidhi hati miliki za ardhi kwa wananchi waliohamia kijiji hicho kutoka Ngorongoro mkoani Arusha pamoja na wenyeji ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akimkabidhi mmoja wa wananchi wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga hati milki ya ardhi tarehe 22 Machi 2023.
"Kijiji hiki sisi kama Serikali chini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tunakwenda kukifanya kama kijiji cha mfano maana yake watu watatoka maeneo mengine kuja kujifunza hapa kutokana na namna kilivyopangwa na mnavyoisimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi," amesema Dkt.Mabula.
Aidha, Dkt.Mabula amewataka wananchi wa kijiji hicho kuepuka migogoro kwa kuwa Msomera ni eneo ambalo serikali inalitupia macho na kujifunza ambapo alisisitiza kuwa wizara yake haitaki kuona panakuwa na vijiji vinavyokuwa bila mpangilio.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati waliokaa) pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga waliokabidhiwa hati milki za ardhi tarehe 22 Machi 2023.
Kwa mujibu wa Profesa Magigi, katika viwanja hivyo kuna maeneo ya huduma mbalimbali ambapo alifafanua kuwa, viwanja vya makazi kila kimoja kina ukubwa wa ekari 2.5 lakini wakati huo huo kukiwa na maeneo ya mashamba yenye ukubwa wa ekari 5 ambapo maeneo hayo yanagawiwa kwa wananchi wanaohamia na wenyeji wa Msomera.