Waziri Kairuki asisitiza walimu kuthaminiwa, kulindiwa utu wao

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki ameisisitiza kila mwalimu nchini aendelee kuthaminiwa na kulindiwa utu wake.
Mheshimiwa Kairuki ametoa wito huo leo Machi 16, 2023 wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika Ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.

"Jambo la Muhimu kwenu ni kuhakikisha mwalimu anathaminiwa na kulinda utu wake. Ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa masilahi ya mwalimu na hadhi yake inalindwa kwa nguvu zote.

"Ni wajibu wetu pia kutambua kuwa mnao mchango mkubwa wa kuwafanya walimu wetu waweze kuleta mabadiliko ya elimu bora nchini kwa kuwahamasisha kutimiza wajibu wao na kulinda masilahi yao pamoja na kuwaondolea kero na malalamiko yaliyo ndani ya uwezo wenu,"amefafanua Waziri Kairuki.

Pia amewataka kushirikiana vema na maafisa elimu wa halmashauri na wathibiti ubora wa elimu katika kumhudumia na kumhamasisha mwalimu kutimiza wajibu wake wa kuimarisha elimu nchini.

"Watumishi wa tume mjitahidi kadri inavyowezekana kuwahudumia walimu shuleni badala ya kusubiri wawafuate ofisini kwenu,"ameagiza Waziri Kairuki.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Kairuki amesema,amezisikia changamoto zinazoikabili Tume ya Utumishi wa Walimu ambazo zimeelezwa na Mwenyekiti wa Baraza, hususani ukosefu wa jengo la ofisi ya makao makuu.

"Nimeona jitihada mlizozifanya na hatua za ujenzi zilishaanza. Pia, nimepata taarifa kuwa mradi wa jengo la tume umeingizwa katika utaratibu wa miradi inayosimamiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, Naibu Waziri Mhe. Deogratius J. Ndejembi amenitaarifu alipotembelea eneo la ujenzi kwamba ujenzi unaendelea chini ya Kandarasi ya SUMA JKT ambapo kasi ya ujenzi imefikia asilimia tano badala ya asilimia 16 kama inavyoonesha kwa mujibu wa Mpangokazi na ameniambia kuwa ujenzi unatarajiwa kukamilika tarehe 5 Juni, 2024.

"Naielekeza Kandarasi ya SUMA JKT ihakikishe kuwa ujenzi wa Jengo la Tume ya Utumishi wa Walimu unakamilika kwa wakati kwa kuwa jengo wanalotumia kwa sasa haliendani na majukumu wanayoyafanya katika kuwahudumia walimu nchini.

"Ili kufanikisha ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi hizi kwa wakati, hakikisheni mnafanya ufuatiliaji na tathimini ya ujenzi wa Mkandarasi huyu kila baada ya mwezi na kunijulisha kila hatua iliyofikiwa na endapo kuna changamoto zinazojitokeza ili tuchukue hatua za kutatua bila kuchelewa,"amesisitiza Waziri Kairuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news