DC atangaza neema kwa bodaboda Pangani

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga imepanga kushirikiana na uongozi wa madereva wa bodaboda kuanzisha Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (SACCOS) ambazo zitakuwa ni kama VICOBA.

Kupitia SACCOS hizo Serikali,bodaboda na viongozi wataweka fedha zao, lengo likiwa ni kuinua vipato vya bodaboda ili kuhakikisha kila dereva bodaboda anamiliki pikipiki yake mwenyewe.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mheshimiwa Zainab Abdallah wakati wa ufunguzi wa uchaguzi wa viongozi wapya wa bodaboda Pangani.

“Uongozi ukipatikana tukae chini tuunde SACCOS ya Bodaboda Pangani ambayo itakuwa kama VICOBA, nyinyi wanachama mna uwezo wa kuchangia mule, Serikali ikipata fedha inaweza kuleta mule,viongozi na wadau wa maendeleo wakipata wanaweka mule.

"Tufanye makadirio tu hapa bodaboda wilayani tupo 1000 mkisema kwa siku muwe na uwezo wa kuchangia shilingi 1,000 maana yake kwa mwezi mnaweza kupata shilingi milioni 30, haiwezekani asilimia kubwa ya madereva bodaboda. Bodaboda hizo ni mali za watu wengine lazima kuwe na malengo ya kuhakikisha wote mnamiliki bodaboda zenu wenyewe,"amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Pia amesema, wakiweka utaratibu mzuri wa kuchanga iwe kila siku au kwa wiki, "na sisi Serikali tukawaunga mkono mtafika mbali, leo nataka niahidi mimi binafsi nitawachangia shilingi milioni 5 kwenye hiyo SACCOS,"amesema.

Mheshimiwa Abdallah amesema, Mbunge wa Pangani ambaye ni Waziri wa Maji,Jumaa Aweso alifanya harambee akachangisha shilingi milioni 65.

"Ameniambia utaratibu wa SACCOS ukikamilika tutaingiza zile fedha kule, zile fedha sio kwa ajili ya watu kujinufaisha na familia zao, umekuwa Katibu hela tumeingiza unaanza kumiliki gari, tunaingiza fedha ili bodaboda wa Pangani wamiliki pikipiki zao wenyewe,"amefafanua Mkuu huyo wa wilaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news