Mgonjwa wa Marburg aliyepona aruhusiwa, Waziri Ummy asisitiza Tanzania ni salama

NA CATHERINE SUNGURA

MGONJWA mmoja wa Marburg mwenye umri wa miaka 26 ameruhusiwa akiwa na afya njema na jamii imetakiwa kumpokea vyema na kushirikiana nae katika shughuli zake. 
Hayo yameelezwa Aprili 4, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Marburg ulioripotiwa Wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

“Ninayo furaha kubwa kuwajulisha kuwa leo tumemruhusu mgonjwa mmoja mwanaume mwenye umri wa miaka 26 akiwa na afya njema, ni matumaini yangu jamii itampokea vyema na kushirikiana nae kama kawaida, ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hatujapata wagonjwa wapya wala vifo.”
Aidha, tangu kuripotiwa ugonjwa huo Machi 21, 2023 kufikia Aprili 4, 2023 jumla ya visa ni 8 na vifo 5.Waziri Ummy ameongeza kuwa, wagonjwa wawili waliolazwa wanaendelea vizuri na matibabu katika vituo maalumu vilivyoandaliwa.

Hata hivyo Waziri amesema kuwa jumla ya watu 212 waliotengamana na wagonjwa wamebainishwa na kati ya hao watu 35 wamemaliza siku 21 za uangalizi bila kuonesha dalili zozote za ugonjwa .
“Hii ni ishara nzuri sana kwetu, Wizara ya afya , serikali na taifa kwa ujumla kwa kuwa maambukizi ya Virus vya Marburg nchini yamedhibitiwa kwa wakati.Serikali bado inahimiza wananchi wote na hasa wa Mkoa wa kagera kuendelea kuchukua tahadhari, kudhibiti na kuzuia maamb ukizi mapya katika jamii”.
Vilevile Waziri Ummy amewahakikishia watanzania na jamii ya Kimataifa kuwa Tanzania ni salama hivyo wananchi waendelee na shughuli na safari bila hofu yeyote na kwamba serikali bado inahimiza wananchi wote hasa wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari kudhibiti ugonjwa na kuzuia maambukizi mapya katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news