Qatar waonesha dhamira ya kuwekeza nchini

NA MWANDISHI WETU

ZIARA ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya mwezi Oktoba, 2022 nchini Qatar imeendelea kuvuta wawekezaji kutaka kuja kuwekeza kwenye sekta ya mifugo hapa nchini.
Hilo limefahamika baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Widam Food, Bw. Al Noubay Al Marri kutoka nchini Qatar kumtembelea Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega jijini Dodoma hivi karibuni.

Akiongea katika kikao baina yake na Waziri Ulega alisema kuwa uamuzi wake wa kutaka kuwekeza hapa nchini ulipata msukumo kufuatia ziara ya Mhe. Rais, Dkt. Samia aliyoifanya nchini Qatar.

Alisema lengo la ziara yake ni kukamilisha hatua za kuanzisha kampuni ya Widam Food hapa nchini ambayo inashughulika na biashara ya Nyama.

"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutufungulia milango ya uwekezaji hapa Tanzania, na sisi tunaona Nyama ya Tanzania ina mustakabali mzuri kibiashara nchini Qatar," alisema Al Noubay

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema Serikali ya Rais Samia imedhamiria kuboresha uzalishaji wa sekta ya Mifugo hivyo ujio wa Mkurugenzi huyo unaunga mkono jitihada za serikali.

"Sisi tunawakaribisha hapa Tanzania, Rais Samia ameshafungua njia, kilichobaki ni sisi kuwawezesha nyinyi ili uwekezaji wenu uweze kufanikiwa," alisema Mhe. Ulega

Aidha, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo pia kumuahidi ushirikiano Mkurugenzi huyo huku akimueleza kuwa akihisi kupata changamoto yoyote asisite kuijulisha wizara ili waweze kuitatua.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news