Rais Dkt.Mwinyi adhamiria mambo makubwa Sekta ya Maji

NA DIRAMAKINI 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendeleza juhudi kuhakikisha maeneo yote ya Zanzibar yanafanikiwa na kufikiwa na maji safi na salama kwa usatawi wa jamii na uchumi wa nchi. 
Picha na Ikulu. 

Hayo yamesemwa leo Aprili 5, 2023 Ikulu jijini Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa tunzo maalum ya watu mashuhuri walioleta mabadiliko chanya katika kuendeleza sekta ya maji Afrika.

Ni tuzo iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Global Water Changemakers kwenye Kongamano la Umoja wa Mataifa nchini Marekani Machi 22, mwaka huu ambayo alikabidhiwa na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Dkt. Mwinyi amesema jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali kuleta mageuzi kwenye sekta ya maji, Zanzibar zitasaidia kustawisha jamii kwa kupatikana huduma za uhakika na endelevu za maji safi na salama. 
“Ahadi yangu ni kuwa Serikali itaendeleza juhudi zake za kuhakikisha maeneo yote ya Unguja na Pemba yanafanikiwa na yanafikiwa kuwa na huduma ya maji safi na salama kwa ustawi wa jamii,”ameahidi Rais Dkt.Mwinyi. 

Amesema, uhaba wa maji nchini unachangia umasikini unaowasababishia watu kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo, hivyo aliahidi serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inayafikia matarajio ya wananchi ya kupata huduma ya maji safi na ya uhakika. 

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza hatua tatu muhimu zitakazoondosha changamoto sugu ya maji Zanzibar endapo zitatekelezwa kwa wakati na watendaji wa sekta hiyo ikiwemo kupanga mipango mizuri na kuitekeleza kwa wakati. 
Pia rasilimali watu wenye uwezo, weledi na ufanisi kutengeneza miradi, kuisimamia na kuitekeleza hadi kuikamilisha kwa msada wa rasilimali fedha ambayo itasaidia kufanikisha mipango waliyojiwekea. 

“Zanzibar ni ndogo tukisema tunalivalia njuga jambo hili kuondoa tatizo la maji Unguja na Pemba inawezekana sana na tutaanza kwa fedha za serikali na baadae kuwaomba wadau wetu kutusaidia ili kukamilisha nchi nzima,” amebainisha. 

Amesema, mpango wa Zanzibar wa uwekezaji wa maji uliandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, kupitia ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu pamoja na mipango ya maendeleo iliyopangwa katika jumuiya za kikanda na kimataifa. 

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi aliipongeza tasisi ya Global Water Partnership Kanda ya Afika Kusini kwa kuwaunga mkono kufanikisha mpango wa uwekezaji wa sekta ya Zanzibar (2022 -2023) ambao umeipatia heshima kubwa hadi kutunukiwa tunzo hiyo kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Zanzibar, na kuongeza kuwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuleta mabadiliko na mageuzi kwenye sekta ya maji Zanzibar. 
Naye Rais Mstaafu, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Maji duniani Kanda ya Afrika ya Kusini, alimpongeza Rais Mwinyi kwa kupokea tunzo hiyo aliyoieleza ni ishara ya jumuiya za kimataifa kutambua jitihada zinazofanywa na Rais na serikali yake kuimarisha sekta ya maji Unguja na Pemba, pia alieleza tunzo hiyo imeipa heshima Zanzibar kimataifa na kuifanya Zanzibar kuwa ni kichocheo cha kuendeleza maji barani Afrika. 

Mpema, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara, alieleza tunzo ya Rais Dkt.Mwinyi ni juhudi alizozifanya ndani ya miaka miwili ya uongozi wake ambapo Serikali imefanikiwa kuzalisha maji lita milioni 149 wakati awali zilizalishwa lita milioni 46 tu za maji. 

Pia kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake Serikali imefanukiwa kulaza miundombinu yam aji kilomita 3,129 wakati awali ilikua kilomita 2001 tu ya miundombinu hiyo. 
Tunzo hiyo maalum ya watu mashuhuri walioleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya maji barani Afrika, yenye lengo la kutambua michango ya viongozi wa Afrika, kuthamini jitihada mbalimbali wanazofanya kwenye masuala ya maji, ilianzishwa na Benki ya Dunia, inafanya kazi zake na Shirika la Kimataifa la Global Water Partership la Sweden ambalo linafanyia kazi zake kwa Kanda tano za Afrika, ikiwemo Kanda ya Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika Kusini, Afrika ya Kati na Afrika ya Magharibi na Dkt.Jakaya Kikwete amepewa dhama ya kuratibu masuala ya maji kwa Kanda ya Afrika Kusini. 

Machi 22, mwaka huu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine wa nchi za Senegal, Namibia, Uholanzi na Zambia walipewa tunzo hizo kwa kutambua mchango wao wa kusimamamia na kuleta mabadiliko chanya katika kuendeleza sekta ya maji duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news