Rais Dkt.Mwinyi:Elimu imepiga hatua kubwa miaka 59 ya Muungano

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, miaka 59 ya Muungano wa Tanzania imeleta mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Elimu kwa pande zote ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ya kisasa na huduma zenye ubora katika kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mwanafunzi wa darasa la saba, Habal Haji Majid wa Skuli ya Msingi ya Kidongochekundu akitoa maelezo jinsi ya kujifunza kupitia Tehama alipotembelea chumba cha kompyuta cha skuli hiyo baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi uliofanyika leo na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa Skuli ya msingi ya kisasa Kidongochekundu iliopo kwenye jimbo la Jang’ombe, Wilaya ya Mjini ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Muungano wa Tanzania. 

Amesema, Zanzibar kwa sasa inastahiki kuwa na skuli za msingi za ghorofa zenye ubora wa hali ya juu ili kuendana na hadhi ya miaka 59 ya Muungano wa Tanzania ambapo Serikali zote mbili ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeshuhudia ongozeko kubwa la taasisi nyingi za elimu na wanafunzi wengi. 
Pia amesema, kabla ya Muungano wa Tanzania, sekta ya elimu ilikuwa na wanafunzi 25, 000 na sasa idadi imeongezeka kufikia 570,000. 

Akizungumzia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ina mpango wa kuongeza madarasa 1000 yenye miundombinu na vifaa vya kisasa zikiwemo maabara, vyumba vya kompyuta, maktaba, vyoo vya kisasa na ofisi za walimu pamoja na kufungua miradi mikubwa zaidi ya maendeleo.
Amesema, mabadiliko ya elimu Zanzibar yatafikiwa kwa kuwa na ujenzi imara wa miundominu ya majengo ya kisasa yatakayochukua wanafunzi wachache kwenye madarasa, vifaa vya kisasa na mazingira mazuri ya kufundisha na kujinza. 

Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa, skuli ya Kidongochekundu Msingi ni miongoni mwa mfano hai wa skuli zote za msingi anazotaka kuzijenga Zanzibar hadi kufikia Januari, 2025 pamoja na kukamilisha miradi mingine mikubwa ya maendeleo ili kuendana sambamba na hadhi ya miaka ya Mapinduzi ya Zanzibar na miaka 59 ya Muungano wa Tanzania. 
“Skuli hii ni mfano wa skuli zetu za msingi nnazotaka ziwe nchini, skuli za ghorofa ambazo ndani yake mna maabara za sayansi, maktaba, vyumba vya kompyuta na madarasa wanafunzi wetu wasiozidi 45,” amebainisha Rais Dkt.Mwinyi. 

Amesema, serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha Zanzibar inapata madarasa ya kutosha, nyenzo bora za kusomea ikiwemo kufanikisha skuli kuwa na mkondo mmoja baada ya miwili kama awali. 
Aidha, amewataka watendaji wa Wizara ya Elimu kuhakikisha skuli inatoa huduma zinazoendana na hadhi yake kwa kutoa ufaulu mzuri kwa wanafunzi. 

Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema, ujenzi wa skuli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025 ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliahidi kujenga miradi malimbali ya maendeleo. 
Ameeleza kuwa, Wizara ya Elimu imepiga hatua kubwa katika kukamilisha miradi yote iliyopanga na kwamba imeakisi dhima ya miaka 59 ya Muungano wa Tanzania. 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Khamis Said amesema ujenzi wa skuli hiyo umegharimu shilingi bilioni 4.466 ambao umejumuisha Maktaba, Maabara, chumba cha kompyuta, ofisi ya mwalimu kuu, ofisi ya msaidizi mwalimu mkuu, ofisi tatu za walimu, chumba cha kusalia, vyoo 25 , viti na meza 1305 kwaajili ya wanafunzi wote. Skuli ya Msingi Kidongochekundu ni miongoni mwa skuli mpya zilizojengwa na Serikali ya Awamu ya Nane kwa fedha za ahuweni ya uviko 19 Zanzibar, kwa Unguja na Pemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news