Thabo Bester (mbakaji wa Facebook) adakwa jijini Arusha

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Tanzania limethibitisha kuwa makachero wa Tanzania wamewakamata raia watatu wa Afrika Kusini ambao ni Thabo Bester (mbakaji wa Facebook), mpenzi wake Dkt.Nandipa Magumana na Zakaria Alberto.

Kwa mujibu wa taarifa fupi iliyotolewa leo Aprili 8, 2023 inadaiwa watatu hao wamekamatiwa Arusha japo taarifa rasmi ya polisi haijasema eneo walikokamatiwa.

Aidha,Msemaji wa Polisi Makao Makuu jijini Dodoma, David Misime amesema taratibu za mawasiliano ya kisheria ya ndani na ya Kimataifa zinaendelea kukamilishwa.

Thabo Bester amekuwa akisakwa na polisi wa Afrika Kusini akikabiliwa na kosa la kughushi kuwa amefariki alipokuwa gerezani na kutoroka kisha baadaye ikabainika kuwa hajafariki, kitendo ambacho kilizua gumzo nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Pretoria leo kupitia mtandao wa APANews,Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini, Ronald Lamola amesema, Bester alinaswa jijini Arusha nchini Tanzania, Aprili 7, 2023 usiku pamoja na mpenzi wake wa Afrika Kusini, Dkt.Nandipha Magudumana na mtu mwingine kutoka Msumbiji.

"Tunaweza kuthibitisha kwamba Thabo Bester na msaidizi wake Magudumana wamekamatwa nchini Tanzania," amesema Waziri Lamola.

Naye Waziri wa Polisi nchini Afrika Kusini, Bheki Cele amesema kukamatwa kwa Bester kuliwezekana kupitia ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi la Afrika Kusini, Jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol) na Polisi wa Tanzania.

"Walionekana wakitoka Dar es Salaam na kufuatwa hadi walipofika Arusha. Ilibainika kuwa walikuwa na hati za kusafiria kadhaa na hakuna hata moja kati ya hizo ambayo imegongwa muhuri nchini Afrika Kusini na Tanzania,"amesema Waziri Cele.

Bester ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela kwa mauaji, alitoroka katika Kituo cha cha Mangaung huko Bloemfontein mwezi Mei, 2022 baada ya awali kuaminika kuwa alijiua kwa kujichoma moto.

Baadaye Idara ya Huduma za Urekebishaji ya nchi hiyo ambayo awali ilitangaza kuwa amefariki, ilithibitisha kuwa mwili uliochomwa moto uliopatikana katika chumba alichokua Bester haukuwa wa muuaji na mbakaji huyo.

Mbakaji wa Facebook alipatikana na hatia mwaka 2012 kwa kuwabaka wanawake wawili na kumuua mmoja, baada ya kuwarubuni kwa kutumia mtandao wa Facebook na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji, wizi na mauaji.

Aidha, Machi mwaka jana maafisa waliripoti kwamba alikufa katika moto katika Kituo cha Mangaung, karibu na Bloemfontein.

Hata hivyo, hivyo baadaye ilionekana Bester alitoroka wakati wa moto na amekuwa akiishi maisha ya kifahari katika kitongoji cha kifahari cha Hyde Park jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news