Goalball, mchezo unaokataza makelele

NA ADELADIUS MAKWEGA 

KUMFIKIRIA mtu mwingine ni sifa ambayo baadhi ya watu wamejaliwa, huku ikiaminika kuwa duniani sifa hiyo sasa ni adimu mno. Swali kwako wewe msomaji wa Mwanakwetu, je umewahi kumfikiria mtu mwingine kwa jambo zuri lenye manufaa kwake? Huku bila ya wewe kupata chochote kile?. 
Msomaji wa Mwanakwetu ebu tumia hata sekunde 60 kulifikiria hilo kabla ya kuendelea kuyasoma makala haya na ndani ya sekunde 1-60 utapata majibu yako. Je umeyapata majibu? Je umezitumia ipasavyo sekunde hizo 60 kupata majibu hayo? Na majibu yako ni yepi? 

Kama majibu yako ni kweli umewahi kuwafikiria wengine pasipo kupata bakishishi kwa hivyo Mwanakwetu anakupa HEKO yenye PONGEZI TELE na kama hauwajawahi kufanya hivyo basi hiyo Heko na Pongezi zake anabaki nayo mwenyewe kibindoni mwake lakini anakukumbusha kuwa haujachelewa, tumia nafasi yako leo kufanya jambo linaloonesha unawajali wengine. 
Natambua fika msomaji wangu unaweza kujiuliza je Mwanakwetu leo ananini nasi ? 

Wala usiwe na shaka, Mwanakwetu yu michezoni, leo amebaini kuwa mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia kumalizika wapo waliopoteza maisha yao, wapo waliopata vilema vya kudumu kwa viungo mbalimbali, ikiwamo miguu, mikono na macho na kuwa vipofu wa milele.Waliopata vilema hivyo walikuwa wakipambana katika vita hivyo kulinda amani ya wengine. 
Ndugu hao kabla ya vita hivyo walikuwa wakishiriki michezo kadhaa, lakini vilema walivyopata vitani vikakwamisha kushiriki michezo tena. Je walipaswa kutengwa na jamii zao? Majibu yake yalikuwa hapana lazima iandaliwe aina ya michezo watakayoweza kushikiki wakiwa na upofu uono hafifu.

Ndugu Hanzi Lorenzen wa Australia na Sepp Reindle raia wa Ujerumani, mwaka 1946 walikuja na majibu ya mchezo huo kwa vipofu na wale wenye uono hafifu mchezo huo ukaitwa Mpira wa Kengele au “Goal ball”. 

Huku Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania inaamini kuwa mchezo huu umechezwa kwenye mashindano ya 20 ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) mwaka 2021 yaliyofanyika kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, Pwani.Mchezo huu ni mchezo mgeni mno kwa Mwanakwetu, nayeye hafahamu kama msomaji wake ni unautambua zaidi yake. 
Hivyo Mei 19, 2023 alipata bahati ya kuona Wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wakijifunza uchezaji wake, hapo ulivyokuwa ukifundishwa na mkurufunzi wa mwaka wa pili wa Stashahada ya michezo chuo hapo Mwalimu Juma Ramadhani Mtimba ambaye pia mwalimu kutoka Shule ya Msingi Ikungi, wilayani Ikungi mkoani Singida, huku kibindoni akiwa ni pia ni mchezeshaji (refa) wa mchezo wa Goal ball wa Taifa. 

“Kila timu inakuwa na wachezaji wanne, ambao kati yao watatu wanakuwa kwenye kikosi cha kwanza na mmoja anakuwa mchezaji wa akiba, wanaoanza mmoja anakuwa mchezaji wa kati na wachezaji wawili wa pembeni.

"Huyu mchezaji wa kati mara nyingi anakuwa yule mwenye hisia za haraka za kubaini mpira pale unapokuwa umerushwa golini kwao na anapoudaka hatakiwi kuugusa zaidi ya mara mbili, akishagusa mara mbili anapaswa kumpa mchezaji wa pembeni akigusa mara ya tatu hilo ni kosa, mchezaji wa kati ambaye ni muhimu kwa ulinzi anapougusa mpira kwa kuwa ni mchezo wa wasioona, anapaswa kufanya ishara ya kugusa mpira kwa nguvu kidogo ili kengele itoe sauti kumwashiria yule wa pembeni kuwa anampa pasi. 

"Akiugusa mara ya tatu hilo ni faulo, na faulo za mpira wa kengele ni kupigwa kwa penati, wakati wa upigaji wa penati wachezaji wa pembeni wanapaswa kutolewa na kubaki yule wa kati peke yake, mpira wa kengele hauna kona wala mpira wa kurusha, goli linapofungwa timu iliyofungwa ndiyo inaanzisha mpira kutoka pembeni mwa goli lao na mchezaji atakayetoa nje mpira unapelekwa kuanzwa kwenye lango la timu pinzani.” 
Hali ya uwanja huwa na vipimo vyake ambapo Mwalimu Mtimba anasema kuwa una urefu wa mita kumi na nane na upana wa mita tisa. 

“Sisi tunachezesha kwa kutumia madarasa na mabwalo, humo tunafanya vipimo alafu wanafunzi wanacheza Mpira wa Kengele Vizuri sana, mchezo huu ifahamike kuwa unachezwa mashuleni hasa katika shule zenye wanafuzni wenye mahitaji maalumu. Vipimo vya viwanja vyake urefu ni mita 18 na upana ni mita tisa. Mpira wake unauzwa shilingi laki tatu na nusu na gharama ya vitambaa ni shulingi laki moja na sabini na tano tu. Huku kipenga chake ni kile kile cha michezo miingine.” 

Mwalimu Mtimba kwa kuwa alikuwa uwanjani akifundisha mchezo huo kipenga chake kilikuwa shingoni kwake , huku akisema bayana kuwa filimbi zikipigwa mara tatu yaani Piii, Piii na Piii hiyo maana yake ni unaanza mchezo kwa dakika 24, Piii Piii maana yake Goli, Piii maana yake mpira umetoka nje.Piiiii maana yake mapumziko na Pii mpira umekwisha.

Akiwa anafundisha somo la mchezo huu mkurufunzi Mtimba alisema kuwa ni vizuri wakurufunzi wanaposimamia mchezo huo wawe watulivu maana mpira wa Kengele wachezaji wake waweze kusikia mlio wa kengele ya mpira mchezoni. 
Huku akiongeza kuwa washangiliaji wanaruhusiwa kwa sharti la kuwa watazamaji tu bila kushangilia hadi pale goli litakapoingia ndipo wanaruhusiwa kupiga makofi tena kwa sekunde chache tu. Alisisitiza kuwa mpira wa kengele hautaki kelele Tofauti na michezo mingine timu zinaweza kushangilia kwa vifaa mbalimbali. 

Wakatia somo hilo la Mpira wa Kengele linafikia ukingoni Mkurufunzi Mtimba alitoa nafasi kwa wanachuo wenzake kuuuliza maswali kadhaa; 

Mimi nauliza hivi mchezo huu tunaruhusiwa kucheza bila viatu? “Mchezo huu unaweza kucheza bila viatu, unaweza kuvaa soksi kama ukivaa viatu tambua unaweza kumkanyaga mwezako na akaumia, nia ya mchezo wetu ni kuucheza na wachezaji watoke bila ya kuumizana kwa hivyo viatu haviruhusiwi kabisa.” 
Kwa nini benchi la wachezaji wa akiba halirusiwi kuhamasisha wachezaji wenzao waliopo mchezoni? Mkurufunzi Mtimba alijibu kuwa hoja kubwa ya mchezo huu hauhitaji kelele ili kuacha mchezo uendelee kama kawaida na kutambua matukio yanayaoendelea mchezoni na wachezaji wasikie sauti ya mpira na ishara nyinginezoza mchezo huu. 

Somo hilo lilipokamilika naye Mwanakwetu akaamua akusimulie kidogo alilolipata katika mchezo huu wa Mpira wa Kengele “Goal ball” Mchezo Unaokataza Makele 

0717649257 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news