Rais Dkt.Samia akubali kurejesha nyongeza ya mishahara

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amekubali kurejesha nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi kwa mwaka nchini.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameyabainisha hayo leo Mei 1, 2023 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) Kitaifa. 
 
Pia amesema hajatangaza kiasi cha fedha au asilimia ya fedha zitakazoongezwa kwenye mishahara ya wafanyakazi mwaka huu ili kuepuka wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa kwa kigezo cha kwamba mishahara imepanda.

“Nawashukuru TUCTA mara hii wamenielewa na hawakuja na mdomo mkali unaotoa moto, mara hii wamekuwa wapole, kwa hiyo wafanyakazi kile watu walichozea tukiseme hapa ili wapandishe bei madukani mara hii hakuna tunakwenda kufanya mambo polepole.

“Wasione tumeongezeana kitu gani ili mwenendo wetu wa bei uwe salama kwa hiyo mambo mazuri yapo ila hatutoyatangaza hapa, lakini wafanyakazi mambo ni moto mambo ni fire, mambo mazuri sana.”

Ni maadhimisho ambayo mwaka huu wa 2023 yameongozwa na kauli mbiu ya "MISHAHARA BORA NA AJIRA ZA STAHA NI NGUZO KWA MAENDELEO YA WAFANYAKAZI, WAKATI NI SASA."
 
Mheshimiwa Rais, pia amewasihi wafanyabiashara kutoongeza bei madukani na kuwaahidi wafanyakazi kuwa mambo mazuri yanakuja pasipo kutangaza hadharani nyongeza hiyo.

“Mishahara kwa mwaka huu mbali na upandishaji wa posho nilizosema tumejiandaa pia kupandisha madaraja, vyeo vitaendelea kupandishwa, kutenganisha makundi na madaraja mserereko wale ambao hawakupata mwaka jana watapata mwaka huu.

“Niseme pia kuna nyongeza za mishahara ya mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa, nikaona kwa mwaka huu tuzirudishe kwa wafanyakazi wote kuna nyongeza za mishahara tunaanda na tutaendelea kama tulivyokuwa tunafanya zamani,”ameeleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Pengine hii huenda ikwa ni habari njema zaidi kwa watumishi wengi wa umma nchini, baada ya kukaa muda mrefu bila nyongeza hizo kutokana na uamuzi uliochukuliwa mwaka 2016 wa kuondoa mfumo huo na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Rais Samia Dkt.Samia amesema kuwa,mwaka jana 2022 Serikali ilipandisha mishahara kwa asilimia 23.3 ambayo si kila mtu alifaidika ila lengo ilikuwa kuwainua wa kima cha chini na wengine wachache, na kuna kundi la walio wengi ambao hawakuguswa na hatua hizo.

“Nikiwemo mimi mfanyakazi namba moja. Lakini kingine tulipandisha posho za wafanyakazi na waliofaidika kwenye hili ni wafanyakazi wenye mishahara mikubwa ambao hawakufaidika na ile nyongeza za mishahara ya asilimia 23.3.

"Nafahamu kuna baadhi ya taasisi hawakuweza kulipa tulipotoa posho tayari bajeti zilishapita kwa maana hiyo mavuno yatakuja mwaka huu,”amesema.
 
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema maombi ya wafanyakazi kwa Serikali waliyoomba mwaka jana ikiwemo kuongezwa mishahara, kupandishwa madaraja na mengine yametekelezwa kwa 95 na sehemu ndogo iliyobaki Serikali inaendelea na utekelezaji.

“Siku chache zilizopita nilikuwa na kikao na Vyama vyote vya Wafanyakazi pale Ikulu kusikiliza wanayokuja nayo mwaka huu, lakini na kuangalia utekelezaji wa mwaka uliopita, nashukuru TUCTA walitoa shukrani kwa tuliyoteleleza.

“Katika yote yaliyotajwa mwaka jana ikiwemo uundwaji wa mabaraza ya taasisi 40 za umma, kulipwa mafao kwa wakati kwa wastaafu na waliondokewa kazini kwa vyeti feki, kupunguzwa kiwango cha kodi ya mapato ya PAYE kutoka asilimia 9 hadi 8 na kuongezeka kwa mshahara na mliomba kuondoa tozo kwenye mihamala kibenki, kupandisha madaraja ya watumishi, kuongezwa umri wa mtoto kuwa mwanachama wa NHIF.Mambo yote mliyoyataka mwaka jana Serikali imetekeleza kwa asilimia 95 na wafanyakazi ni mashahidi."

Mei 14, mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambapo shilingi trilioni 1.59 zilitumika kwa ongezeko hilo.

Hayo yalibainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus ambapo ilifafanua kuwa,mapendekezo hayo ni mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alichokifanya awali mkoani Dodoma na kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu kuhusu ongezeko la mishahara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ilipanga kutumia kiasi cha shilingi trilioni 9.7 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa,taasisi na wakala za Serikali.

“Bajeti ya mishahara ya mwaka 2022/23 inaongezeko la shilingi trilioni 1.59 sawa na asilimia 19.51 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/22,”ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo mwaka jana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news