SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-23

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...makutano walibaki wakishangaa miujiza hiyo iliyofanywa na nabii wa mungu, wachawi waliendelea kumiminika.

Endelea

Pande zote nne za uwanja huo zilitumiwa na wachawi kuingia eneo hilo, wakati huo mtoto THE BOMBOM alikuwa akizunguka toka eneo moja kwenda jingine.

Walinzi wake walikuwa imara kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawa, hakuna mtu aliyepaswa kumsogelea tena mtoto huyo pasipo ruhusa yake.

Wachawi waliendelea kumiminika kama uji wa kibogoyo mdomoni mwake, waliengezeka kila sekunde iliposogea. Washuhudiaji wa tukio hilo walikuwa wengi mithili ya siafu ama nzi kwenye mzoga.

Lilikuwa ni tukio la ajabu kutokea katika historia ya kijiji hicho, walikuwepo wachawi wa aina mbalimbali. Walikuwepo vikongwe, watu wazima, watu wa makamo na vijana.

Ghafla kelele zikatamalaki eneo hilo toka kwa umati huo, hii ni baada ya kumuona shekhe mkuu wa wilaya akiwa juu ya fisi akijongea maeneo hayo kujumuika na wachawi wenzake.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji uchawi ni taasisi kubwa. Taasisi hii inajumuisha watu mbalimbali wamo watu wa kawaida, viongozi wa dini, wanasiasa, wasomi wakubwa nk.

Jambo la msingi unalopaswa kulielewa zaidi ni kuwa, ni vigumu sana mchawi kuacha uchawi. Hakuna mchawi mwenye ubavu wa kuacha uchawi labda kupumzika tu tena kwa kipindi kifupi, hii hutokana na masharti ya dawa zilizoko kwenye mizimu yake kupitia mwilini mwake.

Ikumbukwe kuwa uchawi siyo mwili wa binadamu bali ni mizimu ya mtu mwenyewe ndiyo hubadilishwa na kufuata shughuli hiyo.

Ni vigumu kutenganisha mizimu na mwili wa binadamu, ndiyo maana dawa huchanjwa kwenye mwili, lakini aliyelengwa ni mzimu.

Wapo baadhi ya watu hukataa uchawi wakati wa kurithishwa hii ni kwa sababu ya mizimu yao kuukataa. Hata mchawi anapotaka kukuchukua msukule ni lazima ashughulike kwanza na mzimu wako na siyo mwili wako.

Basi tuendelee,shekhe mkuu huyo wa wilaya alijumuika na wachawi wenzake. Kila mchawi aliyefika eneo hilo alipaki fisi wake na kuendelea kucheza ngoma.

Ngoma ya kichawi hutofautiana toka jamii moja kwenda nyingine, pia hutofautiana toka kundi moja kwenda kundi jingine la wachawi.

Kila kundi la wachawi huwa na ngoma yao ambayo ikipigwa ni lazima wajumuike pamoja. Ndiyo maana mchawi akisafiri mbali na nyumbani kwake, huko huko ugenini ni lazima atapata wachawi wenyeji alikokwenda.

Ngoma za kichawi huwa na faida kubwa kwa mchawi mwenyewe, ndiyo maana huwa wanazipenda sana. Hadi kufikia saa sita mchana kulikuwa na idadi kubwa ya wachawi uwanjani hapo, washuhudiaji wa tukio hilo walikuwa wengi zaidi.

Kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara itokayo Musoma kwenda Mwanza, magari mengi yaliyopita hilo yalisitisha kwanza safari kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo kidogo.

Magari ya kampuni ya Zakaria ndiyo yalikuwa mengi zaidi eneo hilo, yalikuwepo pia magari ya kampuni ya Bunda Bus, Kisire Express, Sabuni, Zuberi Express pamoja na Kalapya Express.

Mtoto yule alisimama kisha akanyoosha mikono yake juu huku macho yake yakiwa yametazama mawinguni. Alizungumza maneno fulani kimya kimya kwa muda wa dakika tano.

Baada ya hapo alisujudu na kuibusu ardhi mara nne, umati ule walifikiri kuwa mtoto huyo alikuwa akifanya mawasiliano na mungu baba.

Watu walikuwa kimya huku wachawi wakiendelea kucheza ngoma yao, ngoma ambayo husikiwa na wachawi tu na siyo watu wengine.

Ghafla kilidondoka kitambaa cheupe kutoka mawinguni, alikichukua kitambaa hicho akapiga magoti tena kushukuru. Miujiza hiyo iliwafanya watu kutahamaki zaidi, kitambaa chenyewe kilikuwa kizito kikiwa katika muundo wa skafu. 

Aliwasogelea wachawi hao na kuanza kuwachapa kwa kutumia kitambaa hicho. Kila aliyeguswa na kitambaa hicho alishituka na kujitambua, uwezo wao wa kuyachakata mambo uliwarudia nakutambua maeneo waliyokuwa.

Ilikuwa ni aibu ya hali ya juu kwa udhalili waliofanyiwa, kisha mtoto huyo akajitia kuwahubiri maneno machache huku akiwataka kuachana na shughuli zao na kumrudia mungu wake.

Kwa kuwa wachawi hao walikuwa wakimfahamu shughuli zake na uwezo wake mtoto huyo waliamua kukaa kimya. Hawakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kuwa wapole, maana kushindana na mtoto huyo isingewezekana.

Nguvu zake zilitabiriwa katika vitabu mbalimbali vya kichawi miaka mingi iliyopita, huyu ndiye nabii mtoto aliyesubiriwa na vizazi vingi vya kichawi vilivyopita.

Baada ya hapo mtoto huyo alianza kuwalaani wachawi hao mmoja baada ya mwingine. Kila mchawi aliyelaaniwa alipotea kwenye mboni za watu, hakuonekana tena yeye na fisi wake.

Laana aliyoitoa mtoto huyo kwa nje ilionekana ni nguvu za mungu, lakini kiuhalisia ilikuwa ni nguvu ya uchawi mtupu.

Mtoto huyo alifanikiwa kupiga ndege wawili kwa jiwe moja, yaani jamii ilimuamini kuwa ni nabii wa mungu wakati huo huo akiwa ameisambaratisha ngome hiyo ya kichawi.

Aliendelea kutoa laana mbalimbali kwa wachawi hao, wapo waliolaaniwa kutopanda gari maishani mwao. Wapo waliolaaniwa kuwa ni marufuku kunyeshewa mvua, wengine walikatazwa kusalimiana na mtu yeyote maishani mwao. 

Wapo waliolaaniwa kutotembea wakati wa giza, wengine laana yao ilikuwa ni jua lisichomoze wakiwa ndani. Wengine ilikuwa ni marufuku jua kuzama wakiwa ndani huku wengine laana yao ni kuhakikisha kila jua linapozama wawe ndani.

Kulikuwa na laana ya kila aina, kibaya zaidi wachawi hao walizuiwa kuendelea na shughuli za kichawi mahali popote. Hili ndilo lilikuwa jambo zito, ni sawa na mtu akuambie ni marufuku kufumbua macho maishani mwako ilihali macho yako ni mazima.

Alipomaliza kazi ya kulaani alipiga magoti, akayainua macho yake juu kisha akamshukuru mungu wake kwa miujiza hiyo.

Wakati anamalizia kuomba kamanda wa polisi wa wilaya,mkuu wa wilaya pamoja pamoja na mkurugenzi walifika eneo hilo.

Kwa kuwa alikuwa amezama kwenye maombi walimuacha akamalizia sara yake, alipofumbua macho yake walikuwa wameshamsogelea zaidi.

Walikwenda kusujudu miguuni mwake huku wakimuelezea namna walivyohangaika kumtafuta siku tano. Wakati huo yule mkuu wa kituo cha polisi Ilongo alikuwepo, uso ulimshuka mithili ya mama mkwe aliyeshikwa ugoni.

Magumu aliyoyapitia ndani ya siku tano ilibaki kuwa siri yake, alimsaka mtoto huyo pembe zote za wilaya, lakini hakumuona.

Hatimaye siku hiyo alifanikiwa kumkuta maeneo hayo akifanya miujiza, mbaya zaidi hata wale watuhumiwa watano alikuwa nao.

Wale viongozi walimuomba mtoto huyo siku mbili baada ya hapo wakutane mji mdogo wa Kanyama ili wamuoneshe eneo alilopewa na serikali kwa ajili ya kufungua taasisi yake.

Mtoto huyo alifarijika kwa kiwango cha juu kusikia habari hiyo. Akiwa kwenye tabasamu hilo ghafla manyunyu ya mvua za rasha rasha yalianza kudondoka eneo hilo, uso na mavazi ya mtoto huyo vilibadilika na kuanza kumetameta. 

Ghafla mbayiwayi mweusi kutoka mawinguni alitua kichwani mwa mtoto huyo. Mara ikasikika sauti kuu toka mlima Ilongo,Ntemi wa mabara! Ntemi wa ng'waleda! Kwa lugha ya kisukuma ilimaanisha mfalme wa dunia.

Watu walibaki wakishangaa sauti hiyo, wapo waliosema kuwa "hakika mtoto huyo alikuwa ni nabii toka kwa mungu" Mambo haya yalifanyika mchana kweupe huku kila mmoja akishuhudia, muda mfupi baadaye hali ya kawaida ilijirudia.

Yule mtoto aliwasogelea viongozi hao akawawekea mikono vichwani mwao kuwatakia baraka, kisha akawashukuru makutano na kuondoka.

Kwa kuwa alikuwa kaambiwa kukutana na viongozi hao eneo la Kanyama hakuona haja ya kuendelea kubaki kijijini hapo hivyo aliamua kuianza safari kuelekea eneo la Kanyama.

Kutoka Ilongo kuelekea Kanyama ni mwendo wa nusu saa kwa gari inayokimbia, lakini kwa mguu ni zaidi ya masaa tano.

Yeye alikuwa amechagua kutembea kwa miguu, lengo lake alitaka kupita maeneo mbalimbali na kufanya miujiza. Makutano waliamua kumfuata mtoto huyo, kila mmoja hakutaka kukosa baraka toka kwa mtoto huyo.

Safari waliianza saa kumi na mbili jioni, idadi ya watu walikuwa wengi mithili ya sisimizi kwenye bua . Ilipofika muda saa moja usiku walikuwa wamefika kijiji cha Kahangala, pale waliwakuta watu wengine wingi wakiwasubiria.

Kila mmoja alitamani kumuona mtoto huyo, japo giza lilikuwa limefunika dunia walikuja na vibatari wengine wakiwa na taa za kandili za kumlika.

Taa za umeme hazikutosha kumlika kundi lile la watu, wazee wa mji wa Kahangala walimuomba mtoto huyo kuzungumza naye japo kwa kifupi.

Idadi ya makutano ilikuwa kubwa hivyo kuendelea kukaa eneo hilo kungepelekea kusimama kwa huduma zingine. Mtoto huyo aliomba kupelekwa nje ya mji eneo lililokuwa na uanda mpana, wazee wa mji huo walimpeleka eneo hilo.

Eneo lilikuwa zuri na pana lenye uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya watu. Mpaka hapo watu walikuwa wamechoka, wengine walikuwa na njaa kwa kuwa hawakuwa wamekula chakula toka mchana.

Wapo waliokuwa na kiu ya maji, lakini hakukuwa na uwezo wa kupata maji. Mtoto THE BOMBOM baada ya kuyaona hayo aliamua kufanya miujiza.

Aliomba chupa ya maji ya dukani moja, mkate mmoja, biskuti pakiti moja na soda za kopo moja. Vyakula hivyo vililetwa mbele yake vikiwa kwenye boksi, alivipokea na kuvinyanyua juu huku akiwa kaangalia uso wake mashariki. 

Alizungumza maneno machache kisha akaviweka chini vyakakula hivyo, ghafla boksi hilo lilianza kuongezeka ukubwa wa umbo na vyakula vikaongezeka.

Ndugu msomaji unadhani vyakula hivyo ni halisi au siyo halisi? Kama ni halisi unadhani vimetoka wapi? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

MAKOYE NKOI

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news