ZIJUE AINA ZA WANASIASA

NA WILLIAM BOMBOM

SIASA na maisha ni sawa na chai na kikombe, huwezi kuzitenga kwa namna yeyote. Ama ni sawa na pande mbili za shilingi ambazo kuzitenganisha ni vigumu.

Picha na vectorstock.

Kwa kuwa siasa hufanywa na mwanasiasa ni muhimu kwa mtu yeyote kutambua aina ya wanasiasa ambao huifanya siasa yenyewe. Zifuatazo ni aina za wanasiasa kwa mujibu wa THE BOMBOM.

A) Wanasiasa mkia wa mbuzi

Wanasiasa wa namna hii huwa ni viherehere sana, wanajua kujipendekeza na kumganda kiongozi kama ruba. Uwezo wao wa kufikiri huwa chini sana kwa maana huwa hawana uwezo wa kujisimamia, zaidi ya kushurutisha na mtu waliyemganda.

Humfuata kiongozi nyuma nyuma mithili ya mkia wa mbuzi, ndiyo maana huitwa wanasiasa mkia wa mbuzi. Hawaangalii uwezo wa kiutendaji kazi wa kiongozi bali huangalia zaidi maslahi wanayoyapata toka kwa mtu waliyemganda.

Wapo tayari kufanya mambo ya hovyo ili kumfurahisha mtu wao, watu hao hawana faida kwa ustawi wa siasa bali wapo kwa maslahi ya mwanasiasa. Hutumika kama tishu kisha kubwagwa mtumiaji anapofanikisha alichokuwa anatafuta.

B) Wanasiasa Wakuda

Hawa ni aina ya wanasiasa wenye roho mbaya sana, kwa kiasi kikubwa wanasiasa wa aina hii hukigombanisha chama kilichoko madarakani na wapiga kura.

Wanasiasa wa namna hiyo huwa kwenye nafasi za chini mfano vitongoji, vijiji au mitaa mpaka kata. Hawa huwasumbua sana watumishi wa serikali kwa kutengeneza majungu na umbeya.

Mara nyingi huwa hawafanyi kazi kwa ajili ya kuingiza kipato chao, kazi zao ni zile za madili kafiri. Wanasiasa wa namna hii hupendelea sana ubaguzi kama udini, ukabila na ukanda.

Sifa nyingine ya wanasiasa wa namna hii, uwezo wao wa kujenga hoja ni mdogo sana maana wengi wao hawajaenda shule na kama alikwenda shule basi alikomea darasa la kwanza au la pili.

C) Wanasiasa mfuko

Hawa ni aina ya wanasiasa ambao huwa wanajiamini sana, mara nyingi hupata nafasi za juu za kuongoza. Kiongozi huwa wabovu sana hawajali matatizo yanayoikumba jamii, wao hutengeneza maisha yao na huwa jeuri sana.

Jeuri yao hutokana na namna walivyopata madaraka, hutumia fedha kuwahonga wahusika au wapiga kura. Ndiyo maana wanaitwa wanasiasa mfuko, maana wametokana na pochi nene kupata madaraka.

Wakifanikisha malengo yao huyeyuka kama barafu kwenye joto, huwa na majibu ya shombo sana wanapoulizwa maswali na raia. Kwa kiasi kikubwa hutumia ndumba na juju kuzima skendo zao mbovu walizozifanya.

D) Wanasiasa asali

Hawa ni wanasiasa ambao hupendwa sana na wananchi kwa kiwango kikubwa, wana maneno matamu mithili ya asali. Silaha yao kubwa ni kusikilizwa, mkimpa muda wa kumsikiliza hasira zenu zinaisha na mtampongeza.

Wana vipawa vya ushawishi walivyopewa na Kalma, ni ngumu sana kuchukia maana ni waumini wa demokrasia. Ni rahisi sana kukuambia sukari ni mchanga na mchanga ni sukari, akijenga hoja ni lazima utakubali.

Hawa ndiyo husababisha watu kujitoa mhanga na kupelekea maafa endapo wataonewa au kugandamizwa. Katika uongozi wao huleta maendelea ya kati ndani ya jamii maana hawapendi kuchukua maamzi magumu yatakayosababisha watu wao walalamike.

Kwa kifupi ni viongozi waliobobea kwenye taaluma ya uongo wa hali ya juu, huwa na marafiki wengi kila kona kulingana na uwezo wao.

E) Wanasiasa maalumu

Hawa ni wanasiasa ambao huandaliwa na chama fulani kisha kupenyezwa kwenye vyama vingine ili kupata taarifa maalumu.

Wanasiasa hawa huwa siyo wasaliti kwa vyama vilivyowaandaa, huwa wamebobea kwa kiwango kikubwa juu ya imani ya vyama vyao, hivyo hata watakapopenyezwa kwenye chama kingine hufanya kazi hiyo maalumu na nyoyoni mwao huendelea kuwa na msimamo thabiti.

Wanapokuwa kwenye vyama walivyopandikizwa hujitahidi kugombea nafasi za kati. Huwa hawajulikani sana ndani ya jamii.

F) Wanasiasa jadidi

Hawa ni aina ya wanasiasa ambao huwa hawana maneno ya kubembeleza. Ni viongozi ambao huchukiwa sana na jamii kipindi wakiwa kwenye madaraka, hawajui kubembeleza mtu zaidi ya kumshughulikia anayekwenda kinyume na utaratibu.

Ni watu wenye kuchukua maamzi magumu juu ya jambo, huipeleka mbele jamii kimaendeleo kwa muda mfupi mno. Ni wachache sana kuwapata ndani ya jamii, hutokea mara chache sana kwa muda mrefu.

Husimamia kwenye hoja wanazoamini, huanzisha miradi mikubwa ambayo na kuimaliza kwa muda mfupi. Huacha alama ndani ya jamii ambayo huzungumzwa miaka mingi.

Huwa na maadui wengi sana kulingana na misimamo yao, wanapotoka kwenye siasa jamii huwalilia sana na kuwaomba angalau warudi.

G) Wanasiasa Simama

Hawa ni aina ya wanasiasa ambao huwa hawabadiliki, husimama imara juu ya vyama vyao hata kama vitapitia nyakati ngumu.

Kulingana na misimamo yao mara nyingi huuawa dhidi ya mahasimu wao, hii hutokana na kutokuwa waoga. Hata kama utawapeleka polisi ama gerezani huwa hawaogopi, ni vigumu pia kiwanunua ili wawe upande wako.

Wapo tayari kuzaliwa na kufia kwenye chama chao hata kama hakuna maslahi, hukaa chama kimoja miaka yote huku wakipambana kufanya mapinduzi dhidi ya maovu yanayotokea ndani ya jamii. Endapo wanafanikiwa kuongoza nchi, hufanya maendeleo kwa muda mfupi, huwa siyo waumini wa visasi.

G) Wanasiasa kha!

Hawa ni wanasiasa ambao mara nyingi siyo waongeaji, hutumia mabavu sana kuongoza jamii. Hufanya mauaji ya hali ya juu dhidi ya watu wanaowapinga, hawana uvumilivu na mtu atakayewakosoa.

Mikono yao imejaa damu za watu hawana huruma hata kidogo, hupenda kuona uhai wa watu ulipotea pasi na sababu. Watu hupigwa risasi mfano wa mnyamapori, wengine hupotezwa mithili ya upepo.

Wapo ambao hufungwa kwenye viroba na kutumbukizwa kwenye kina kirefu cha maji wangali wapo hai. Watu huishi kwa wasiwasi ndani ya jamii yao.

Mara nyingi wanasiasa wa namna hii siyo waumini wa demokrasia. Huponda sana mali za nchi na rafiki zao, mara kwa mara husafiri maeneo mbalimbali nje ya nchi kula bata. Katika uongozi wao rushwa hutamalaki kila eneo, huwa hawaachii madaraka mpaka waondolewe au wafe.

Haya ndiyo makundi ya aina ya wanasiasa, unaweza kupima upo kundi gani au kiongozi wako yupo kundi gani.

WABEJA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news