TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-21:KARIBU RUVUMA,MKOA WENYE FURSA LUKUKI

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Ruvuma unapatikana Kusini mwa Tanzania. Upo kati ya Latitudo 90 35 na 110 Kusini mwa Ikweta, Longitudo 340 31 na 380 10 Mashariki ya Greenwhich.

Aidha, Ruvuma unapakana na Jamhuri ya Msumbiji kwa upande wa Kusini, Ziwa Nyasa upande wa Magharibi na Mkoa wa Iringa upande wa Kaskazini na Kaskazini Mashariki. Pia unapakana na Mkoa wa Mtwara kwa upande wa Mashariki.

Upo katika Nyanda za Juu Kusini kutoka 300m hadi 2000m juu ya usawa wa bahari. Sehemu ya Magharibi ya mkoa imefunikwa na Ziwa Nyasa ambalo liko Magharibi mwa Bonde la Ufa.

Upande wa Mashariki wa Bonde la Ufa kuna safu za Milima ya Matengo ambayo huinuka hadi 2000m. Vile vile kuelekea Kaskazini kuna Milima ya Lukumburu ambayo mwinuko wake upo hadi 2000m kutoka usawa wa bahari. Kusini mwa mkoa unapitia tambarare za chini ambazo zimepasuliwa na mto Ruvuma.

Mbali na kuwa mpaka wa asili kati ya Jamhuri ya Tanzania na Msumbiji, Mto Ruvuma pia ni mto muhimu katika mfumo wa maji Kusini.

Mto Ruvuma unatiririsha maji yake katika Bahari ya Hindi na unaundwa na vijito kadhaa vya kilele kama vile Njuga, Likonde, Ngembambili na Lukimwa.

Mito mingine ni pamoja na Luegu, Mbarang’andu, Lutukira, Ruhuhu na mito mingine mingi midogo midogo pia inaunda mfumo wa kutitirisha maji.

Mkoa wa Ruvuma una jumla ya eneo la kilomita za mraba 64,393 ambapo kilomita za mraba 2,978 zimefunikwa na maji na kuacha eneo la ardhi la kilomita za mraba 61,415.

Kati ya eneo la ardhi kilomita za mraba 54,457 sawa na asilimia 89 ni ardhi ya kilimo na kilomita za mraba 6,958 sawa na asilimia 11 ziko chini ya hifadhi ya misitu. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, Mkoa wa Ruvuma umesheheni fursa lukuki. Endelea;


1. Ruvuma mkoa pia,
Songea ukiingia,
Huko ninakujulia,
Nilipokuwa shuleni.

2. Kilimo ninaanzia,
Mengi wanatufanyia,
Na kama wangesinzia,
Tungekuwa matatani.

3. Mahindi watupatia,
Maghala tunajazia,
Uchumi wapalilia,
Pongezi tunawapeni.

4. Kahawa Mbinga sikia,
Uchumi wanachangia,
Kule ukikupitia,
Kunavutia machoni.

5. Makaa ya mawe pia,
Huko wanajichimbia,
Umeme yazalishia,
Na nishati viwandani.

6. Mbufu nawakumbukia,
Samaki tulijilia,
Nyasa wanawavulia,
Kitoweo majumbani.

7. Tunduru korosho pia,
Tumbaku wapalilia,
Selous inaanzia,
Wa kunyumba asanteni.

8. Miundombinu sawia,
Ruvuma inavutia,
Mambo kulala kwa njia,
Sasa ni ya kizamani.

9. Hapa kwa kumalizia,
Simama kwa kuanzia,
Dakika moja changia,
Wahenga tukumbukeni.

10. Waliotupigania,
Majimaji kumbukia,
Kweli walitushindia,
Kwa damu yao na mali.

11. Mimi ninakumbushia,
Vita walipigania,
Majimaji nakwambia,
Walishupaa vitani.

12. Ukombozi lichangia,
Ingawa walifulia,
Nguvu tulizipatia,
Mbele kusonga vitani.

13. Habari kifwatilia,
Songea tazikutia,
Elimu tajipatia,
Mwanzo na hata mwishoni.

14. Mmoja nakutajia,
Mama aliyetishia,
Mrembo nakutajia,
Nduna Nkomanile yani.

15. Chifu limsaidia,

Mioyo hamasishia,
Vita kuvipigania,
Kwa ukombozi nchini.

16. Sifa yake kisikia,
Ya pekee nakwambia,
Alivyotupigania,
Kujitia kitanzini.

17. Nduna peke nakwambia,

Mwanamke lipitia,
Kunyongwa akaishia,
Huyo shujaa nchini.

18. Wadachi limzimia,
Hamasa litufanyia,
Ingawa aliishia,
Fahari kubwa nchini.

19. Yeye twamfagilia,
Livyotuhamasishia,
Lindi na Mtwara pia,
Wote kuenda vitani.

20. Kama hujamsikia,
Ndio leo nakwambia,
Kumbukumbu kipitia,
Yaingie akilini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news