Ujumbe kutoka DRC watembelea Bandari ya Dar es Salaam

NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayesimamia majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, Bw. René Kalala Masimango na ujumbe wake upo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo Mei 4,2023 ulikutana na Uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) jijini Dar Es Salaam.

Akizungumzia kuhusu ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Mshana alisema ubalozi wake umeiandaa kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa Tanzania na DRC ili wajadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Wakati wa kikao na uongozi wa TPA, Bw. Masimango alisema Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa mizigo ya Congo na inahudumia mizigo mingi, hivyo ziara yake ni kujionea utendaji kazi wa Bandari na ameridhika kuwa kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo ni nzuri na zimepangiliwa vizuri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa ameahidi kuwa Menejimenti yake ipo tayari kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza katika kuhudumia shehena ya mizigo inayoenda na kutoka Congo kupitia Bandari za Tanzania kwa lengo la kulinda uhusiano mzuri na wa muda mrefu wa kidiplomasia na biashara kati ya nchi hizi mbili.

“Menejimenti ya TPA itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zozote katika kuhudumia shehena ya Congo na kuimarisha uhusiano ili shughuli zinazofanywa na TPA katika bandari zake ziwe na manufaa kwa DRC,”Alisema Bw. Mbossa.

Naye Balozi wa DRC nchini Tanzania, Mhe. Jean Pierre Massala amesema ziara hiyo ni muhimu kwa uhusiano kati ya DRC na Tanzania na muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja kwa faida ya nchi hizi mbili. Ujumbe huo wa DRC unaendelea na ziara yake nchini na leo tarehe 05 Mei 2023 umepanga kutembelea Bandari Kavu ya Kwala na Reli ya Kisasa ya SGR.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news