Zanzibar yadhamiria makubwa kupitia Sekta ya Elimu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali imedhamiria kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu kupitia wizara yake ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo Vijana ili waweze Kujiajiri na Kuajirika katika Sekta ya Uchumi wa Buluu, uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja jijini Zanzibar leo Mei 17,2023. (Picha na Ikulu). 

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 17, 2023 kwenye ufunguzi wa mradi wa kuwajengea uwezo vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri na kuajirika kwenye sekta ya uchumi wa buluu huko ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Dkt.Mwinyi amesema, Serikali inaendeleza jitihada mbalimbali kwa kuhakikisha inatoa elimu bora nchini katika kufikia dhamira hiyo kwa kuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya skuli mpya ikiwemo ujenzi wa skuli mpya za ghorofa kwa Unguja na Pemba na mafunzo kwa walimu.

Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali itahakikisha inazipatia huduma muhimu skuli hizo ikiwemo, upatikanaji wa vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia, matumizi bora ya TEHAMA na kuwapatia vijana ujuzi na maarifa utakaowawezesha kuyakabili maisha yao na kunyanyua uchumi wa nchi.
“Kama hatutowaandaa vijana wetu, wakawa weledi wa kujua wanachokifanya, hatutofikia dhamira yetu ya kuhakikisha watu wote wakiwemo vijana wanashiriki na kunufaika na Uchumi wa Buluu,”ameasa Rais Dkt.Mwinyi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi,alitaja sehemu ya ujenzi wa mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chuo cha kisasa cha Ubaharia na majengo ya utawala, ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa kike kwenye Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume yenye ukubwa wa ghorofa tatu.

Sambamba na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 500 kwa wakati mmoja, ujenzi wa madarasa ya kusomea na karakana zinazohusiana na masomo ya mafuta na gesi.
Ameongeza kuwa,pia kuna ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya amali na vifaa vyote vinavyohitajika kwa programu zitakazotolewa na vyuo hivyo ambavyo vinatarajiwa kujengwa kwenye Wilaya za Mkoani (Chambani), Wilaya ya Micheweni (Tumbe Mashariki), Wilaya ya Kati (Jendele) na Wilaya ya Kaskazini B (Panga Tupu).

Shughuli nyingine za mradi huo wa SEBEP, Rais Dkt.Mwinyi alizitaja ni pamoja kuwajengea uwezo watendaji wa taasisi zinzozoshiriki kwenye mradi huo kwa kuwapatia nafasi za kuongeza taaluma zao, ujenzi wa kituo cha kuwapa vijana mafunzo ya kuanzisha na kuendeleza biashara zao na vifaa vyake eneo la Kizimbani Unguja, ambacho kitakuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) na Taasisi ya SMIDA imepewa jukumu la kuwapatia mafunzo mbalimbali vijana hao.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, hatua hiyo inatoa nafasi kwa vijana wa Zanzibar kupata fursa ya mafunzo ya amali na ufundi wa fani mbalimbali zikiwemo zinazohusiana na Uchumi wa Buluu.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa vijana kuitumia vyema fursa ya mradi huo kujipatia ujuzi ili wanufaike na soko la ajira kwenye sekta ya uchumi wa buluu kwa kuweza kujiari na kupata sifa za kuajiriwa.

Dkt.Mwinyi amesema, mradi huo utaongeza upatikanaji wa wafanyakazi wenye taaluma kwenye shughuli za utalii ambayo ni sekta kiongozi katika uchumi wa Zanzibar pamoja na kuiwezesha Zanzibar kuzitumia vyema rasilimali zake za asili ikiwemo bahari, mafuta na gesi asilia katika kukuza pato la taifa na upatikanaji wa ajira kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu.

Mradi wa kuwajengea uwezo vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri na kuajirika kwenye Sekta ya Uchumi wa Buluu (SEBEP) unafadhiliwa kwa asilimia 90 na washirika wa maendeleo (AfDB) na asilimia 10 unafadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na unatarajiwa kutumia dola za Marekani milioni 54 sawa na fedha za Tanzania shilingi bilioni 126.379.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news