Tanzania yapaa Kimataifa katika kutoa huduma za matibabu ya moyo

NA MWANDISHI WETU

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itaendelea kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa nchi zinazoizunguka Tanzania ili huduma hiyo iweze kuwafikia watu wengi zaidi na kuokoa maisha yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.

Dkt. Kisenge alisema Taasisi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ikiwemo Malawi lakini kutokana na uhitaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nchini humu wakaona ni vyema waratibu kambi ya upimaji na matibabu ya moyo na kuwatuma wataalamu wa JKCI kwenda kutoa huduma kwa wananchi wa Malawi.

“Kwa namna ya kipekee ninamshukuru aliyekuwa Balozi wa Malawi Mhe. Humphrey Polepole ambaye alitufuata na kutuomba tukatoe huduma za matibabu ya kibingwa nchini humo kwani kuna uhitaji mkubwa wa huduma hiyo na aliichagua Taasisi yetu kwa kuwa inatoa huduma bora za matibabu ya moyo hapa nchini na katika nchi za Afrika Mashariki na Kati”.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpongeza Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya pamoja na timu ya wataalamu wa Taasisi hiyo waliokwenda nchini Malawi katika Hospitali ya Queen Elizabeth kwaajili ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo.

“Baada ya wataalamu wa Taasisi yetu kwenda kutoa huduma nchini Malawi imeonekana kuna wagonjwa wengi wanaohitaji kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwani huduma hizo hazipatikani nchini humo hivyo basi ni nafasi kwa Tanzania kwenda kutoa huduma nchini Malawi na katika nchi za jirani ambazo hazina huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.

“Wagonjwa hawa baada ya kufanyiwa uchunguzi wamepewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu ambako ni karibu na Malawi ukilinganisha na nchi zingine. Kwa kuja kwao hapa nchini nchi yetu itaongeza mapato pia tutakuwa tumeutangaza utalii wa matibabu ambao ni maelekezo na maono ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi yetu iwe ni mahali ambapo watu watatoka katika nchi mbalimbali na kuja kupata huduma za matibabu”, alisema Dkt. Kisenge.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema licha ya kwenda nchini Malawi kutoa huduma za matibabu ya moyo, hivi sasa wanaratibu na kuandaa kambi za matibabu ya moyo ili waweze kwenda kutoa huduma katika nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Visiwa vya Comoro kwa kufanya hivyo wataweza kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitaji huduma hizo.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza katika hafla fupi ya kuwapongeza madaktari bingwa wa moyo waliokwenda kutoa huduma za upimaji na matibabu katika Hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo nchini Malawi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye alikuwa mkuu wa msafara wa wataalamu waliokwenda kutoa huduma nchini Malawi Dkt. Angela Muhozya alisema wagonjwa waliowaona walikuwa wanahitaji huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Dkt. Angela alisema wakiwa nchini Malawi walitoa huduma za matibabu kwa watoto na watu wazima ambapo wengi wa wagonjwa walikuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, matundu, valvu za moyo na mishipa ya damu ya moyo kushindwa kupitisha damu vizuri.

“Tulifanya upimaji kwa wagonjwa 724 kati ya hawa waliokuwa na matatizo ya moyo ni 537. Waliohitaji rufaa walikuwa 201 kati yao 132 watafanyiwa upasuaji wa moyo watoto wakiwa 78 na watu wazima 54 na waliohitaji kufanyiwa uchunguzi na upasuaji kwa njia ya tundo dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab walikuwa 69 kati ya hao watoto 36 na watu wazima 33”.

“Wagonjwa 15 tuliwapa rufaa ya haraka kwaajili ya kufanyiwa upasuaji mkubwa au mdogo wa moyo,”amesema Dkt.Angela.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Stella Mongela alisema watoto wengi waliowaona walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake na wengine walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuambukiza ambayo ni Valvu za moyo kushindwa kufanya kazi vizuri.

“Watoto wengi walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo hata watoto wa hapa nyumbani wanayo, tofauti iliyopo ni hapa nchini huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana lakini kule huduma hizo hakuna na hivyo wagonjwa kushindwa kupata huduma kwa wakati,”amesema Dkt. Stella.

Dkt. Stella aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa na taasisi ya moyo yenye vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wa kutosha kwa kuwa na huduma hiyo kunawasaidia watanzania wakiwemo watoto kupata huduma za matibabu ya kibingwa kwa wakati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news