DCEA yaja na operesheni kabambe mipakani kudhibiti dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeanza operesheni shirikishi na jumuishi katika mipaka mbalimbali ya nchi ili kuwezesha kudhibiti uingizwaji na utoaji wa dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 9, 2023 na Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo wakati akiendelea na ziara katika Mpaka wa Horohoro jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati hiyo kabambe nchini.

"Tuko hapa Horohoro kwenye mpaka ambao ni mkubwa,na unapitisha bidhaa mbalimbali. Na hii ziara tulianza katika Mpaka wa Namanga tumeenda katika mpaka wa Tarakea, mpaka wa Holili na sasa tupo mpaka wa Horohoro.

"Tuna operesheni mbalimbali tunazoziendesha hapa nchini na katika operesheni zetu tumebaini kwamba dawa za kulevya sasa hivi zinapita katika mipaka na baada ya Serikali kuweka miundombinu mizuri, na ya kisasa katika viwanja vya ndege sasa hivi wale wasafirishaji wa dawa za kulevya hawana tena nafasi ya kusafirisha dawa za kulevya kupitia viwanja vya ndege."

Kuhusu DCEA?

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha Novemba 8, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Aidha, Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, Machi 24,2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi Septemba 15, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu Februari 18, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Kamishna Jenerali tena

Wakati huo huo, Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo ameendelea kufafanua kuwa, "Sasa hivi dawa nyingi zinapitia kwenye mipaka, kwenye nchi kavu, lakini pia baharini.

"Kwa hiyo sasa hivi tunachokifanya tunahakikisha kwamba tunatembelea kwenye mipaka yote ili tuhakikishe kwamba tunajenga mahusiano mazuri, tunajenga ushirikiano na taasisi zote za Serikali zilizoko katika mipaka ili kuhakikisha kwamba tunafanya operesheni ya pamoja kwenye mipaka yote.

"Lengo ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti dawa za kulevya kuingia nchini, dawa za kulevya ni uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka ambao unatoka nchi nyingine kwenda nchi nyingine,kwa kushirikiana na taasisi za Serikali zilizoko kwenye mipaka yote ambapo zipo taasisi 17 kwenye kila mpaka, tutahakikisha tunafanya operesheni za kutosha kuhakikisha tunadhibiti dawa za kulevya zisiingie nchini, lakini pia zisitoke nchini kwenda nchi nyingine.

"Lakini, pamoja na kufanya hii operesheni tutatoa elimu pia kwa maafisa wote wa taasisi za Serikali zilizopo mipakani ili waelewe pia aina mbalimbali za dawa za kulevya ambazo zinasafirishwa, lakini pia wajue mbinu mbalimbali ambazo zinatumika kusafirisha hizo dawa za kulevya, ili tuwe na uelewa wa pamoja na tuweze kufanya operesheni za pamoja.

"Lakini pia pamoja na hiyo elimu, tutatoa pia elimu ya kisheria, baada ya sheria yetu kubadilishwa na kuimarishwa zaidi, ili pia waelewe sheria yetu inasemaje kuhusiana na dawa za kulevya. lakini pamoja na elimu hiyo tutakayoitoa kwa maafisa wetu kwenye mipaka yote tutatoa pia elimu kwa jamii zilizoko mipakani ili watusaidie katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya katika jamii na mipaka.

"Kwa sababu dawa za kulevya nyingi zinavuka mipaka iliyo rasmi, kwa sababu Serikali kwenye hii mipaka imeweka miundombinu mizuri, imeweka midaki ambayo inakagua bidhaa zote ambazo zinapita kwenye mipaka, lakini wale wasafirishaji wa dawa za kulevya wanapita nje, wanachepusha na wanapita nje ya mipaka.

"Ili jamii ipate elimu kuhakikisha kwamba wanapata elimu ya dawa za kulevya na wanatambua pia mbinu ambazo wanatumia wale wasafirishaji wa dawa za kulevya ili wao wawe sehemu yetu ya kutupa taarifa na kubaini pia ile mitandao inayochepusha hizi dawa za kulevya, ili iturahisishie pia kwenye operesheni zetu tunazozifanya.

"Lakini, Tanga ni eneo moja wapo ya eneo ambalo linaoongoza kwa dawa za kulevya, usafirishaji wa dawa za kulevya, lakini pia matumizi ya dawa za kulevya, kwa hiyo niwaambie pia wananchi wa Tanga hasa wale wasafirishaji wa dawa za kulevya, waache wenye kabla ya kukabilwa na hatua kali za kisheria,"amefafanua kwa kina Kamishna Jenerali Lyimo.

Majukumu

Majukumu ya Mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya. Katika kutekeleza majukumu hayo Mamlaka inafanya kazi zifuatazo:

i.Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya.

ii.Kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya.

iii.Kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii;

iv.Kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya;

v.Kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti;

vi.Kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

vii.Kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi;

viii.Kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

ix.Kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa;

x.Kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya;

xi.Kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xii.Kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya;

xiii.Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu.

xiv.Kufanya uchunguzi wa sayansi jinai

Wafanyabiashara

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara kutoka katika maeneo hayo wamesema, "kuhusiana na uingizwaji wa dawa za kulevya, ni kwamba Serikali ina haja iweze kutufikia wananchi wa mazingira haya ili iweze kutupa elimu, kwamba ni namna gani na jinsi gania mbavyo tunaweza kushiriki kusaidia kudhibiti dawa za kulevya zisiweze kuingia katika nchi yetu.

"Hivyo, Serikali ina nafasi ya kutupa elimu wananchi tuweze kudhibiti hilo, pia sisi kama wafanyabiashara wa eneo hili tupo tayari kushirikiana na Serikali ili tuweze kudhibiti dawa za kulevya yasiweze kuingia katika nchi yetu, kwa sababu yana uwezo wa kuendelea kuangamiza vizazi vyetu,"amefafanua mmoja wa wananchi na wafanyabiashara katika maeneo ya Horohoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news