Dkt.Mayrose Kavura Majinge afunguka kuhusu Kongamano Tiba la Afya ya Akili nchini

NA GODFREY NNKO

MRATIBU wa Kongamano-Tiba la Kitaifa la Afya ya Akili ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Family Vibes Foundation, Dkt.Mayrose Kavura Majinge amesema, Julai 11, 2023 katika Uwanja wa Uhuru uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wameandaa Kongamano Tiba la Afya ya Akili ambalo litawakutanisha wadau mbalimbali wakiwa na majawabu kuhusu changamoto hiyo ya kiafya.

Wataalamu wa afya wamethibitisha kuwa,magonjwa ya akili ni matatizo ya ubongo ambayo humfanya mtu kuwa na hisia, fikira na matendo tofauti na yale yanayotarajiwa na jamii na kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha.Magonjwa ya akili yanaweza kusababishwa na sababu za kibaiologia au kisaikolojia.

Dkt.Majinge ameyasema hayo leo Juni 25, 2023 wakati akizungumza na DIRAMAKINI jijini Dar es Salaam kuelezea kuhusu maandalizi ya kongamano hilo kubwa.

"Baada ya kongamano tarehe 11, Julai kuanzia tarehe 12, Julai mpaka mwezi wa 10 kabla ya tarehe 10, 2023 tunatafuta timu ya wafikiriaji angalau 20, tutakaa na hizo changamoto zote ambazo tutaletewa tutakaa na kuzitafutia majawabu na suluhisho, halafu ile siku ya kilele cha Afya ya Akili Duniani tarehe 10 mwezi wa 10 tutatoa majibu hayo kwa pamoja;

"Kwa hiyo, Julai 11, mwaka huu tutakuwa na Kongamano Tiba la Afya ya Akili, litafanyikia Uwanja wa Taifa wa Uhuru uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

"Litakuwa linawaalika watu mbalimbali kwa sababu ni Kongamano Tiba la Afya ya Akili, sasa unajua sisi tuna-promote afya bora ya akili kama watu wanavyo-promote afya bora ya mwili, kwa sababu hauwezi kuwa na afya bora ya mwili kama akili ina shida.

"Kwa hiyo, tuna-promote afya bora ya akili, hivyo pale kutakuwa kuna mada maalumu itakayojadiliwa katika kongamano hilo, inayosema Dhibiti Magonjwa Yako kwa Afya ya Akili.

"Na tayari hiyo mada tumeshaiweka katika kitabu ambacho tunakisambaza ili siku ile ya tukio, watu wakija pale inakuwa ni maswali, majibu, maoni, ushauri na way foward,tumefanya hivyo ili kuwapa nafasi washiriki waweze kupata suluhisho zaidi ya changamoto inayowakabili kuliko kuanza kuwafundisha watu kama wako darasani.

"Kwa hiyo pale litakuwa ni kongamano tiba baina ya mtu mmoja mmoja, mazungumzo tiba kupitia maswali ya watu ambayo yametokana na hiyo mada au mchakato wenyewe wa afya ya akili, changamoto za afya ya akili, wanapouliza basi wanapata tiba,"amefafanua Dkt.Majinge.

Wakati huo huo, Dkt.Majinge amebainisha kuwa, "Pale pale watapata msaada wa tiba, japo siyo wote kwa sababu tunaendelea kusambaza vitabu vyenye hiyo mada na pia mawazo tiba ili watu waanze kupata tiba wakiwa huko.

"Lakini pia waweze kushiriki kwa wingi kwa sababu siyo raihisi watu wote wanaweza kufika uwanjani,lakini watapata hizo mada kupitia kitabu ambacho tumeanza kukisambaza kwa wadau mbalimbali ili waweze kukipitia kabla ya ile siku.

"Kwa hiyo tunaalika wadau wote ili waweze kushiriki, na siku hiyo watakuwepo wataalamu wa afya ambao watawawezesha kupima afya zao bure, madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali hapa Dar es Salaam watakuwepo wakiwemo kutoka Ocean Road, Temeke, Ilala, Mwanayamala na hata Hospitali ya Taifa Muhimbili watakuwepo,"ameongeza Dkt.Majinge.

Kwa nini Family Vibes?

Dkt.Majinge amefafanua kuwa, Family Vibes Foundation inashughulika na afya ya akili kinga, "kwa sababu,tunatoa elimu pamoja na ushauri ama mazungumzo tiba kuhusu watu wenye mambo magumu, yaani watu wanaokabiliana na mambo magumu, siku hizi wanasema kuvurugwa.

"Kwa hiyo, kama mtu jambo lake anakosa mahali au anakosa majawabu hao tunawasaidia, tunawapa huo ushauri na mazungumzo tiba, hivyo baadaye wanakuwa sawa, siyo kwamba wanaacha zile changamoto zao, hapana wanakabiliana nazo kwa namna ambayo haiathiri afya yao, haiathiri kazi zao, lakini pia haiathiri mahusiano yao na wengine, unajua mtu akishavurugwa anaweza kukosa hata hamu ya kula.

"Sasa unapokosa hamu ya kula utapata wapi nguvu, ya kufanya kazi yako ina maana utaathiri kazi yako, lakini unapokosa hamu ya kula chakula, unaathiri afya yako, kwa hiyo unakuta ile changamoto inasababisha afya yako kuathirika.

"Lakini pia inasababisha shughuli yako kuathirika vile vile ukiwa una changamoto fulani,mwingine unakuta anakuwa ana hasira,lakini pia hana amani, unajua ukiwa hauna amani, mwili unakuwa hauna nguvu hata kuongea ile unakuwa hauwezi kuchangamka, kwa hiyo hali hiyo inasababisha hata mahusiano na watu wengine yanakuwa siyo mazuri.

"Kwa hiyo, sisi tunasaidia mambo kama hayo, kwa hiyo mtu anapozungumza anakuwa huru, anamwaga ile sumu, hivyo anapata nafuu na anakuwa sawa katika maisha yake.

"Sasa, katika shughuli hizo tumeona kwa kweli hali imezidi, watu wanazidi kwa sababu ya maisha magumu, watu wanazidi kuwa na hizo hali kwa sababu kuna kukosa amani, kukosa furaha, kuwa na msongo wa mawazo.

"Kwa, hiyo sasa kutokana na hali hiyo tukaona tutengeneze programu kubwa itakayotengeneza uelewa wa pamoja ili kusaidia angalau tuweze kupunguza ile hali kwa watu wengi.

"Unajua, hasa hasa sisi tunashughulika na kuhamasisha afya bora ya akili, kama vile watu wanavyohamasisha afya bora ya mwili,"amesisitiza Dkt.Majinge.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news