Serikali yaendesha doria kali dhidi ya simba waliozua taharuki Iringa

NA JACOB KASIRI 

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeungana na timu ya Mkoa wa Iringa kushiriki katika doria ya kuwasaka wanyama aina ya simba ambao hivi karibuni walizua taharuki katika vijiji jirani na hifadhi.
Kupitia doria hiyo, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema ameungana na timu hiyo kushiriki doria ya kuwasaka wanaosemekana wametoka katika maeneo yao ya asili na kuvamia vijiji vilivyoko jirani na Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuua mifugo kitu kinachosababisha taharuki katika maeneo wanayozurura.

Akizungumzia kuhusiana na tukio hilo, Kamishna Mwakilema amefafanua kuwa, "Nilipata taarifa ya uvamizi wa wanyama hao katika vijiji vilivyoko mbali kabisa na hifadhi zaidi ya kilomita 25.
"Lakini hadi sasa simba hao wameshaenda umbali wa zaidi ya kilomita 70 na wameshavuka barabara ya lami ya kutoka Morogoro, Iringa kwenda Mbeya na wako upande wa pili wa barabara wakiendelea kufanya uharibifu.

"Baada ya uvamizi wa wanyama hao,timu ya askari 17 kutoka Hifadhi ya Taifa Ruaha na maafisa kutoka Kanda ya Kusini walifika kwa haraka kushirikiana na wenzetu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, TAWA (Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzani) na KDU (Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu) kuwasaka simba hao wasilete madhara zaidi," amesema Kamishna Makilema.
Aidha, Kamishna Mwakilema amesema kuwa, kutokana na unyeti wa jambo hili walifanya jitihada za kupata helikopta.

"Na jana wasaidizi wangu wameruka nayo ila kutokana na hali halisi ya milima na makorongo marefu hawakuweza kuwaona. 

"Pia nimeongea na mtu wa AWF pale Manyara Ranch ili kuweza kupata mbwa wa kunusa watusaidie kutambua harufu za simba hao,"amesema Kamishna huyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy amesema kuwa wilaya imeingiwa na taharuki kubwa baada ya kupata taarifa ya uwepo wa simba katika Kata ya Magoma na kuua ng'ombe. 

"Kwa haraka niliwasiliana na wenzetu wa TANAPA na TAWA kuja kuwaondoa simba hao.Hata hivyo, Simba hao waliendelea kusonga mbele wakiua mifugo na hatimae kufika eneo la Kiponzelya karibia na mji wa Iringa. 
"Hadi kufika Juni 24, 2023 simba hao wameshaua ng'ombe 25, na kujeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu, pia wameua mbuzi watano, kondoo watano, nguruwe watatu na kuku mmoja," aliongeza mkuu wa wilaya huyo.

Mkazi wa kijiji cha Tanangozi, Grayson Laurent Mtende amesema, "baada ya kupata taarifa za simba kijijini kwetu tuliogopa kwa sababu simba hawazoeleki na ni mnyama anayeogopwa hivyo tumesitisha kufanya kazi zetu mashambani kwa muda mpaka pale mamlaka zinazohusika na uhifadhi zitakapotuambia hali ni shwari."
Simba hao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya watano bado hawajaonekana na jitihada za kuwasaka zinaendele kwa kutumia magari, helikopta na jitihada za kupata mbwa wa kunusa zinaonesha kuzaa matunda. 

Pia wananchi wanaendelea kuelimishwa njia salama za kujilinda na wanyama kwa kutokuwaruhusu watoto na watu wazima kwenda vichakani kuokota kuni, na wanapotoka nje nyakati za usiku watoke na tochi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news