Habari kubwa za Magazeti ya Tanzania leo Juni 3,2023


Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC),Bw.Samwel Kamanga na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 365 likiwemo shtaka la kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya shilingi bilioni moja mali ya NIC.

Mashtaka mengine mbali na kuongoza genge la uhalifu ni kughushi, kutoa nyaraka za uongo, kuchepusha fedha na utakatishaji wa fedha na kulisababishia shirika hilo hasara.Hata hivyo, Mahakama imewasomea washtakiwa hao mashtaka 101 tu, kabla ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Juni 6, 2023.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Ipyana Mwakatobe akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga imewataja washtakiwa wengine mbali na Kamanga kuwa ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa zamani wa NIC, Tabu Kingu, wahasibu Victor Mleleu, Peter Nzunda, Kenan Mpalanguro, Lisubilo Sambo na Mfworo Ngereja.

Katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu imedaiwa Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Evodia Kyaruzi kuwa, washtakiwa walitenda kosa hilo kati ya Januari Mosi, 2013 na Desemba 31, 2018 katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam mkoani Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Kigoma.

Inadaiwa katika kipindi hicho washtakiwa kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia sh. 1,863,017,400.76 kwa njia ya ulaghai kutoka Shirika la Taifa la Bima. Kesi hiyo itaendelea Jumatatu, Juni 5, 2023 watuhumiwa wamerudishwa mahabusu.










Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news