Kasulu yapokea walimu 139 ajira mpya, wanne waingia mitini

NA RESPICE SWETU

ZIKIWA zimetimia siku zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa watumishi wapya wa kada ya afya na ualimu kuripoti katika halmashauri walizopangiwa, imefahamika kuwa jumla ya walimu 139 wameripoti katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Mwalimu John Malugu wa Shule ya Sekondari Asante Nyerere akipokea maelekezo kutoka kwa Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) Wilaya ya Kasulu, Samwel Rubamba (aliyesimama) wakati wa kukamilisha taratibu za ajira.

Akitoa taarifa ya kuripoti kwa walimu hao, Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu Wilaya ya Kasulu, Samwel Rubamba amesema, idadi hiyo inajumuisha walimu wa shule za msingi na sekondari.

Amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu iliyopangiwa walimu 143 kati yao 115 wakiwa ni wa shule za msingi na 28 wa shule za sekondari, imepokea walimu 139 hadi kufikia Juni 22, mwaka huu muda uliowekwa kwa watumishi hao wa ajira mpya wawe wameripoti.

Amefafanua kuwa, kati ya walimu waliofika, walimu 113 ni walimu wa shule za msingi na 26 wakiwa ni walimu wa sekondari.

"Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ilipangiwa walimu 143 wa ajira mpya ambapo hadi jana waliokuwa wameripoti ni 139 wakisalia wanne ambao kati yao wawili ni wa shule za msingi na wawili wakiwa ni wa sekondari,"amesema.

Rubamba amewataja walimu ambao hawajaripoti na shule walizopangiwa kuwa ni Adeliph Bwemero wa Kamembe na Sukaina Gulamali wa Rusesa huku Adam Msigwa na Ramadhan Samatta wote wakiwa wa Shule ya Sekondari ya Kamuganza.

Kuhusu hatima ya walimu ambao hawajaripoti amesema, walimu hao walipewa muda maalumu wa kuripoti kwenye halmashauri walizopangiwa, muda ambao umetamatika pamoja na juhudi kubwa zilizofanyika za kuwatafuta walimi hao.

"Maafisa elimu wamefanya kazi kubwa sana ya kuwatafuta walimu hao kwa kuwapigia simu na kwa njia mbalimbali hawakupatikana, nitumie nafasi hii kuwaasa walimu hao wajitokeze ili kunusuru ajira zao,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news