Rais Dkt.Mwinyi aendelea kufanya maboresho ya kisasa serikalini

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya kieletroniki katika ukusanyaji wa mapato.

Sambamba na mazingira ya kufanyia kazi kwa ujenzi wa ofisi za kisasa, upatikanaji wa vitendea kazi na utoaji wa mafunzo kwa watumishi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyti ameyasema hayo leo Juni 24, 2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Zanzibar na kuzindua mifumo mitatu ya kieletroniki ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-Wakil jijini Zanzibar.

Ameeleza kuwa, Serikali italinda na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kila hali ya uchumi itakaporuhusu na kupandisha pensheni kwa wastaafu na tayari imeanza utaratibu mpya wa kulipa pensheni jamii kwa mwaka huu.

Tangu Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi ilipoingia madarakani jumla ya mifumo 28 ya kieletroniki imetengenezwa kwa kuongeza ufanisi katika uwajibikaji na utoaji wa huduma bora.

Mifumo mitatu imezinduliwa rasmi leo ikiwa ni pamoja na mfumo jumuishi wa taarifa za watumishi na malipo ambao utakuwa na mchango mkubwa wa uwekaji na uhifadhi wa taarifa za watumishi na kurahisisha mwenendo wa miamala ya fedha kwa kudhibiti wizi wa fedha za Serikali.

Vilevile mfumo wa Zan Ajira ni muhimu katika kurahisisha shughuli mbalimbali zinazohusu ajira na kuimarisha misingi ya usawa.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa watumishi wote kuitumia mifumo yote iliyoanzishwa ili kuleta tija iliyokusudiwa na kuimarisha ufanisi katika Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi pia ameuhimiza uongozi wa wakala wa Serikali mtandao uongeze kasi katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma.

Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaziimarisha taasisi zote zinazoshughulika na usimamizi wa utawala bora ikiwemo Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar (ZAECA), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) na Tume ya Maadili kwa Viongozi wa umma kwa kuzipatia nyenzo na mafunzo ili ziweze kusimamia kwa ufanisi zaidi masuala yanayohusu uwajibikaji, uadilifu, uwazi, upatikanaji wa haki na huduma bora kwa wananchi na kutunga sheria mpya zinazohitajika ili kuzipa nguvu zaidi taasisi hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news