Rais Dkt.Mwinyi awashukuru wadau wa maendeleo

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inajivunia ushirikiano wake na wadau wa maendelo likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Elimu na Watoto Duniani (UNICEF).

Hayo yamebainishwa Juni 6, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipozungumza na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF Tanzania, Bi.Shalini Bahuguna aliyefika Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi kwenye shirika hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akikabidhi zawadi ya Mlango wa Zanzibar kwa mgeni wake Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF nchini Tanzania, Bi. Shalina Baguhuna,alipofika Ikulu jijini Zanzibar akiwa na Ujumbe wake katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Dkt. Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na timu nzima ya UNICEF Tanzania kupitia ushirikiano wake, kwani wako bega kwa bega katika kuimarisha masuala yanayohusu ustawi wa watoto nchini.

“UNICEF imefanya makubwa Tanzania hususani ushirikiano wake wa karibu katika kuiunga mkono Serikali yetu kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo, wamefanya mengi siwezi kuyaonesha maeneo yote sababu ni mengi mno,”amefafanua Rais Dkt. Mwinyi.

Pia Dkt.Mwinyi amempongeza Bi.Shalini kwa jitihada zake, kwa kipindi chote alichofanya kazi na UNICEF hapa nchini akieleza mchango mkubwa walioutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na shirika hilo katika kuiunga mkono SMZ.

Rais Dkt.Mwinyi alimweleza Mwakilishi huyo kwamba, daima Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulishukuru Shirika la UNICEF kwa kuiunga mkono Zanzibar kwenye masuala ya Afya na Elimu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bi.Shalini alimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa uongozi wake hasa katika kuzisimamia vema rasilimali za Zanzibar kwenye ujenzi wa maendeleo ya Wazanzibari wa maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Alimsifu Dkt.Mwinyi kuwa Kiongozi wa mfano hasa kwa kukinawirisha kimaendeleo Kisiwa cha Pemba na mageuzi makubwa aliyofanya kwenye sekta za afya na elimu Zanzibar.

Vilevile, Bi.Shalini ameisifu za Zanzibar kwa kufanikiwa kutekeleza malengo ya Milenia kwani imefanikiwa kwenye suala zima la kudumisha usafi wa mazingira kwa maeneo mengi ya miji.

Akizungumzia mafanikio katika ustawi wa masuala ya watoto, Mwakilishi huyo wa UNICEF aliipongeza Serikali ya Dkt.Mwinyi na kueleza kuwa Zanzibar imefanikiwa kwa asilimia 75 kuwarejesha skuli watoto wengi walioacha masomo kwa mazingira tofauti waliyokumbana nayo kwenye makuzi yao.

UNICEF ni Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) lililoanzishwa tangu mwaka 1946 jijini New York nchini Marekani, linashughulika na masuala ya Elimu na Watoto duniani,linafanya kazi kwenye maeneo zaidi ya 190 duniani kote, katika kuwafikia watoto na vijana walio kwenye matatizo kutokana na majanga mbalimbali kwa kuboresha chanjo kwa watoto na kutoa lishe bora katika kuimarisha huduma za dharura mbali na mambo mengine yanayowahusu watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news