Tanzania, Kenya zajadili kuboresha mahusiano katika Sekta ya Nyumba na Makazi

NA MWANDISHI WETU
Nairobi Kenya

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo, Dkt.Angeline Sylvester Lubala Mabula amekutana na Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Kenya,Bw. Zachariah Mwangi Njeru na kufanya mazungumzo yanayolenga kuboresha uhusiano wa mataifa hayo mawili katika sekta ya nyumba na maendeleo ya makazi.
Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Kenya, Bw. Zachariah Mwangi Njeru akizungumzia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu wa Taifa hilo jijini Nairobi leo.

Waziri Mabula amesema kuwa Serikali ya Tanzania ipo makini katika kusimamia maendeleo ya sekta ya nyumba na makazi ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu mijini linalofikia asilimia 4.8 kwa sasa. 

Amebainisha kuwa, moja ya juhudi za Serikali ni utekelezaji wa mpango wa miaka 10 wa kurasimisha makazi holela ulioanza mwaka 2013.

Pia amesema kuwa, ili kuwapatia watanzania nyumba bora, Serikali ilianzisha Shirika la Nyumba la Taifa, ambalo kwa kushirikiana na wadau wengi wanaendelea kupunguza uhaba wa nyumba unaofikia nyumba milioni 3.8 hivi sasa.

Amesema kuwa, wizara yake iko mbioni kuanzisha mfuko wa kusaidia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kutafuta teknolojia itakayosaidia ujenzi wa nyumba nyingi kwa bei nafuu. 

Kuhusu uimarishaji wa mipaka ya kimataifa, Waziri Mabula aliuambia ujumbe wa Kenya kuwa Tanzania inaendelea kuweka alama za mipaka hizo kwa kushirikiana na wataalam wa Kenya na kazi inaenda vizuri.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Kenya wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Zachariah Mwangi Njeru amesema kuwa nchi yake imeanzisha mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambao utawezesha ujenzi wa nyumba laki mbili kila mwaka.

Amesema kuwa, mpango huo utashirikisha sekta binafsi na ili kufanya nyumba hizo kuwa na gharama nafuu Serikali ya Kenya wataweka miundombinu ya umeme na maji, imeondoa asilimia 16 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya vifaa vya ujenzi na uuzaji wa nyumba na wameanzisha mfuko wa nyumba utakaochangia kwa asilimia tatu na kila mtumishi wa sekta ya umma na binafsi na asilimia tatu nyingine itachangiwa na kila mwajiri. 

Wakihitimisha mazungumzo yao, mawaziri hao wamekubaliana kuunda Kamati ya Wataalam wa pande zote watakaosimamia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo yaliyosainiwa mwaka 2021 jijini Dar es Salaam. 
Waziri Dkt. Mabula akishiriki kikao cha Mawaziri wa Afrika wanaosimamia nyumba na makazi kilichoketi Jijini Nairobi.

Wakati huo huo, kikao cha Mawaziri wa Bara la Afrika wanaosimamia nyumba, makazi na mazingira kimekubaliana kuongeza uwekezaji wa fedha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuweka mpango madhubuti wa kupunguza idadi ya watu mijini, kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuwa na sauti moja kama Afrika ya kuondoa changamoto za makazi na mazingira. 

Akizungumza katika kikao hicho cha Mawaziri wa Afrika, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amesema kuwa, Bara la Afrika linapaswa kuongeza vitendo zaidi katika kupunguza makazi holela, uharibifu wa mazingira na kuwapa uelewa wa kutosha wananchi ili kupunguza athari hizo. 

Amefafanua kuwa, Serikali ya Tanzania imekuwa na mipango madhubuti ya kuboresha makazi na kusaidia upatikanaji wa nyumba.

Mkutano huo wa Shirika la Makazi Duniani unaoendelea jijini Nairobi utafungwa kesho kwa kupitishwa maazimio kadhaa yanayolenga kuisaidia dunia kukabiliana na uhaba wa nyumba bora, kuondoa makazi holela na mabadiliko ya tabianchi, kama yanavyosisitizwa na ajenda ya shirika hilo ya kuwa na malengo endelevu ya miji kufikia 2030.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news