Tanzania kutoa tamko leo kuhusu makazi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

NA MWANDISHI WETU
Nairobi-Kenya

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula ambaye anamuwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN-Habitat) atawasilisha tamko la Tanzania leo. 

Tamko hilo litaonesha juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kukabiliana na changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi, kama sehemu ya malengo ya milenia ambayo kila nchi duniani inatekeleza.
Waziri Mabula atatoa tamko hilo leo Juni 6, 2023 jijini Nairobi nchini Kenya kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN-Habitat) unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 5,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkutano huo unafanyika wakati Dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za makazi zilizosababishwa na UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya kivita ambayo imeongeza hali ya umaskini, huduma hafifu za makazi, njaa na mafuriko katika maeneo kadhaa ya dunia. 

Waziri Dkt.Mabula ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri duniani wanaohusika na uendelezaji wa miji na makazi. 

Mkutano huo ulitanguliwa na mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani ulioanza Juni 5, 2023 jijini Nairobi ambao kauli mbiu yake ni "hatma ya miji endelevu kupitia ushirikishwaji na uwepo wa mifumo ya mahusiano ya kimataifa."
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN-Habitat), Bi.Maimunah Mohd Sharif ameeleza kuwa, kufikia mwaka 2030 watu bilioni 3 ambayo ni asilimia 40 ya idadi ya watu duniani watakuwa wakiishi mijini katika makazi yasiyo salama na yasiyokiwa na huduma muhimu. 

Hivyo, ili kukabiliana na hali hiyo nchi zote za dunia zinapaswa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto zitakazotokana na kuongezeka kwa idadi ya watu. 

Bi. Maimunah ameyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba ya utangulizi ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe.William Samoei Ruto kufungua mkutano huo. 

Bi Maimunah amesema kuwa, changamoto hizo zinahitaji serikali zote za dunia kushiriki kikamilifu kukabiliana nazo ili kufikia malengo ya milenia ya kuwa na miji endelevu, salama na jamii imara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news