TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-27: KARIBU TANGA, UPENDO NA FURSA

NA LWAGA MWAMBANDE

KWA mujibu wa andiko la Tanga Initiative and Mindset Organization, historia inaonesha kuwa,Mkoa wa Tanga una eneo la kilomita za mraba 27,348 na uko Kaskazini Mashariki mwa Tanzania ukipakana na Kenya upande wa Kaskazini.

Pia, Bahari Hindi upande wa Mashariki na mikoa ya Morogoro, Manyara na Kilimanjaro. Mpaka upande wa Kusini unafuata Mto Mligaji. Mkoa wa Tanga unaunganisha sehemu za Pwani pamoja na milima ya ndani kama Usambara.

Kuna wilaya 10 ambazo ni Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini, Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini.

Eneo linalofaa kwa kilimo ni kilomita za mraba 17,000. Aidha, Tanga ni kati ya mikoa midogo ya Tanzania ikiwa na msongamano mkubwa wa wakazi ndani ya eneo lake.

Jina hili la mji wa Tanga lilitokana neno la Kiajemi lenye maana nne tofauti ambazo ni: Iliyo nyooka; Bonde lenye rutuba; Barabara upande wa mto na Shamba juu ya mlima, neno hilo hilo la Tanga kwa kabila la Kibondei ambalo ni wenyeji wa mkoa huo linamaana ya shamba, wao hulitamka N'tanga.

Tanga inasamekana imeanzishwa na wafanyabiashara Waajemi katika karne ya 14. Mji wa Tanga haikupata umuhimu kama mji wa jirani ya Mombasa. Tarihi ya Pate inasema kwamba kabla ya kuja kwa Wareno Pate iliwahi kutawala Lindi kwa muda fulani.

Katika karne ya 19, Tanga ilikuwa chini ya utawala wa Omani na Zanzibar. Misafara ya biashara imeanzishwa hapa kwenda bara.

Kutokana na bandari yake nzuri ya kiasili Tanga ilikua sana wakati wa ukoloni wa Wajerumani waliojenga bandari wa kisasa pamoja reli kwanda Moshi.

Reli iliwezesha kilimo kwa ajili ya soko la dunia Tanga ikawa bandari kuu kwa jili ya katani na kahawa. Baada ya Uingereza kuchukua utawala wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani reli ya Tanga-Moshi iliunganishwa na ile ya kati hivyo ikawa na njia kwenda Dar es Salaam pia.

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Tanga iliona mapigano makali Novemba 3 hadi 5,1914. Jaribio la Uingereza kuvamia Tanga kwa kikosi cha askari 8000 Waingereza na Wahindi kutoka meli kwenye Bahari Hindi ilishindwa vibaya na Jeshi la Ulinzi wa Kijerumani chini ya uongozi wa Paul von Lettow-Vorbeck.

Mwaka 1922 "Tanganyika Territory African Civil Services Association" (TAA) iliundwa Tanga ambalo lilikuwa shirika ya kwanza ya Kiafrika lenye shabaha za kisiasa.

Kwa jumla, Tanga hali ya hewa ni joto lenye unyevu. Handeni kuna joto ikiwa pakavu zaidi. Milima ya Usambara hapana joto sana.

Miezi ya Desemba hadi Machi hali joto huko Tanga inafikia sentigredi 30-32 mchana na 26-29 usiku. Wakati wa Mei hadi Oktoba halijota inapoa ni sentigredi 23-28 mchana na 20-24 usiku. Unyevu iko juu kati ya asilimia 100 na asilimia 65.

Maeneo mengi ya mkoa hupokea angalau milimita 750 za mvua kwa mwaka au zaidi. Pwani ni zaidi takriban milimita 1,100 hadi 1,400 mm ikipungua sehemu za ndani isipokuwa milima ya Usambara ambako mvua inaweza kuzidi milimita 2000 kwa mwaka.

Makabila makubwa mkoani Tanga ni Wasambaa, Wazigua, Wabondei na Wadigo. Wasambaa ndio kabila kubwa lililoko katika milimani ya Usambara, Muheza, Korogwe na Lushoto. Kwa jumla ndio asilimia 40 ya wakazi wote wa mkoa.

Wazigua ni kabila kubwa huko Handeni na sehemu za Korogwe na Pangani. Wabondei wako hasa Muheza na sehemu za Pangani. Wadigo ndio wengi Tanga penyewe na sehemu za Muheza.

Msongamano wa wakazi ni mkubwa hasa wilaya ya Lushoto penye ardhi yenye rutuba nzuri. Wilaya ya Handeni kuna machimbo ya madini.

Wakazi wengi mkoani Tanga hutegemea kilimo cha riziki pamoja na ufugaji na uvuvi. Mazao ya chakula hasa ni mahindi, mihogo, ndizi, maharage na mpunga.

Mazao ya biashara ni katani, pamba, kahawa, chai, nazi, tumbaku na korosho. Mifugo ni ng'ombe, mbuzi na kondoo pamoja na kuku.

Katani ilikuwa zao la biashara hasa kwa ajili ya Tanga tangu kuingizwa kutoka Mexico zamani za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Hulimwa kote mkoani isipokuwa Lushoto, hasa Muheza na Korogwe kwenye mashamba makubwa.Mashamba haya yalikuwa ya walowezi, yalitaifishwa baada ya uhuru.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema pia, utalii umeanza kupanuka kwa kasi na shughuli za uwekezaji mkoani Tanga. Endelea;


1. Tanga ninakutajia,
Mkoa ulotimia,
Wenyewe wanatambia,
Upendo wamesheheni.

2. Wasema ukiingia,
Huko waweza bakia,
Sifa ninatamania,
N'kajionee machoni.

3. Uhuru kupigania,
Walishatuandikia,
Kimweri alipofia,
Ni Tanga siyo Manyoni.

4. Amboni ukisikia,
Ni mapango fwatilia,
Jinsi waliyatumia,
Kajifunze ubaini.

5. Joto pwani lazidia,
Lushoto ni baridia,
Nazi na bandari pia,
Tanga utaitamani.

6. Kwa uchumi Tanzania,
Tanga sana yachangia,
Bandari twashabikia,
Kwa shehena za thamani.

7. Mradi twasubiria,
Bomba la mafuta pia,
Kutanoga nakwambia,
Pwani ya Chongoleani.

8. Viwanda si makasia,
Tanga tunajivunia,
Saruji vyatufanyia,
Tunajengea nyumbani.

9. Sabuni kusafishia,
Na zile za kufulia,
Viwanda vyatupatia,
Tuwe wasafi njiani.

10. Zao kuu zamania,
Na halijachikichia,
Pande nyingi twatambia,
Tanga hadi Kigamboni.

11. Mkonge twashangilia,
Umejenga Tanzania,
Dola ulitupatia,
Hasa miaka sabini.

12. Hutengeneza gunia,
Na kamba za kufungia,
Wengine wanatumia,
Mazuria majumbani.

13. Mkonge umechangia,
Tanga watu kufikia,
Watu waso asilia,
Huko Tanga washeheni.

14. Leo utawasikia,
Watu Njombe asilia,
Mbeya walikoanzia,
Kuishia mikongeni.

15. Kazi walifwatilia,
Kabla ya Tanzania,
Tena walivyofikia,
Wamekufanya nyumbani.

16. Sishangae kusikia,
Akina Mwakusikia,
Huko wameshasalia,
Kama wako kitaluni.

17. Penzi ushalisikia,
La Tanga naulizia?
Huko ukishaingia,
Huondoki asilani.

18. Kupenda nawasifia,
Hutoki ukiingia,
Wengi wanawasifia,
Nchini na ugenini.

19. Waja leo mesikia,
Homu wakutulizia,
Yale wanakufanyia,
Unabakia chumbani.

20. Ukibanwa nakwambia,
Kuondoka fikiria,
Majaliwa nakwambia,
Tanga takuwa nyumbani.

21. Faru lishawasikia?
Huko tawaangalia,
Mkomazi natajia,
Ndiko waishi mbugani.

22. Ni adimu nakwambia,
Wachache wamesalia,
Twalinda twapigania,
Ili wabaki nchini.

23. Chai ukijitakia,
Tanga utajipatia,
Nyingine twaitumia,
Twala fedha za kigeni.

24. Mto Pangani sikia,
Umeme watupatia,
Uvuvi twautumia,
Mtoni na baharini.

25. Muheza umesikia?
Korogwe umefikia?
Matunda yamejazia,
Twayafaidi nchini.

26. Lushoto nako pitia,
Vema utajisikia,
Kulivyo ninakwambia,
Ni bora sana nchini.

27. Baridi inazidia,
Kama wanafukizia,
Kutalii nakwambia,
Kuzuri ni kileleni.

28. Taka jipumzikia,
Ndege wakikuimbia,
Ni Lushoto kimbilia,
Utakuwa kivulini.

29. Mahitaji mengi pia,
Kwa kuwekeza ingia,
Hoteli twahitajia,
Kuwakarimu wageni.

30. Tanga nitakurudia,
Siwezi kusingizia,
Mengi nayakumbukia,
Nikitaja ulimini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news