Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) waja na tabasamu kubwa kwa wanafunzi wa kike nchini

DAR ES SALAAM-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) chatangaza udhamini wa masomo katika kozi ya msingi kwa wasichana waliokosa fursa ya kujiendeleza katika masomo ya sayansi.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hiki anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Deus Ngaruko, ametangaza fursa hiyo Julai 22, 2023, wakati wa Maonyesho ya Sayansi na Teknolojia alipotembelea banda la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“CKHT inatekeleza mradi wa Mabadiliko ya Uchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Chuo hiki kimepewa jukumu la kuinua vipaji vya wasichana ambao kiwango chao cha ufaulu kinakaribiana na wale waliopata sifa za kujiunga na elimu ya juu katika fani za Sayansi, Teknolojia, Hisabati na Uhandisi. Watakaofanikiwa kupata fursa ya kusoma kozi hii maalum ya msingi, watapata ufadhili wa ada na mahitaji mengine,” amesema Prof. Ngaruko.
Aliendelea kusema kuwa, wasichana hao wakishahitimu kozi hii wataweza kuomba na kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha nchini ikiwemo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB).

Aidha, katika kuhitimisha maonyesho hayo ya kumi na nane yaliyoanza kurindima kuanzia Julai 17, 2023 na kuhitimishwa Julai 22, 2023 wageni wengi wameonyesha kufurahishwa na huduma bora iliyokuwa inatolewa katika banda la CKHT.
Bi. Sauda Abdala, akiongea baada ya kupata ushauri katika banda la CKHT na hatimaye kuamua kujiunga na chuo hicho amesema alikuwa hana uamuzi sahihi wa kozi ambayo ingemfaa kutokana na uwepo wa kozi nyingi na vyuo vingi lakini ushauri huo umemuwezesha kufanya maamuzi sahihi.

“Nimekuja kama wateja wengine katika banda lenu, nimekuta banda ni zuri na huduma kwa wateja ni nzuri sana, mlijipanga vyema. Hapa nimeshauriwa vyema na hatimae nimeamua kujiunga na chuo hiki maana sikuwa najua nikasome nini na wapi,”amesema Bi. Sauda.
Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika kila mwaka nchini yanaratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU). 

Aidha,maonesho hayo hukutanisha vyuo na taasisi mbalimbali nchini zilizo chini ya tume hiyo kwa ajili ya kuonyesha na kutangaza huduma zitolewazo na taasisi hizo. 

CKHT ni miongoni mwa taasisi zilizofanikiwa kushiriki katika maonyesho hayo ya kumi na nane.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news